Header Ads Widget

RC KHERI AWAONDOA HOFU WANANCHI OKTOBA 29, AWATAKA WAJITIKEZE KUPIGA KURA.

 

NA MATUKIO DAIMA.

IRINGA. MKUU wa Mkoa wa Iringa Kheri James amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa watahakikisha usalama wa wananchi unakuwa kipaumbele huku haki ya kila mmoja inalindwa kikamilifu ili zoezi la upigaji kura liweze kukamilika vizuri.

Kheri James amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake na kubainisha kuwa wajibu wa serikali ni kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha kabla ya uchaguzi,ndani ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Alisema kuwa wajibu huo wameanza kuufanya vizuri na kila mmoja ni shahidi kwamba mkoa wa Iringa  ni salama mpaka sasa. 

"Mkoa wa Iringa upo tayari kuingia katika uchaguzi kama ambavyo imetangazwa na tume huru ya uchaguzi kwamba uchaguzi utakuwa tarehe 29, oktoba na hivyo wananchi woyte wenye sifa za kikatiba watakuwa na uhuru na nafasi ya kushiriki katika zoezi hilo"

Aidha amewahakikishia wananchi kwamba maeneo yote yatakayotumika katika upigaji kura kwa maana ya vituo vya upigaji kura yatakuwa salama wakati wote.

Maeneo ya huduma katika mji huo yatakuwa salama wakati wote, viunga vyote vya kuingia na kutoka katika mji huo wa Iringa vitakuwa salama.

"Niwatoe mashaka kwamba pamoja na jukumu la watu kupiga kura lakini huduma zingine na shughuli zingine zitakuwa na uhakika wa usalama wakati wote"alisema 

"Jukumu la usalama ni la wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama na kila mdau muhimu wa maendeleo ya Mkoa wa Iringa anatakiwa kulisimamia kwa ushiriano ili mkoa uwe salama wakati wa uchaguzi, ndani ya uchaguzi na baada ya uchaguzi"

Pamoja na hayo RC Kheri amewahakikishia utayari wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kushughulikia changamoto ambayo inaweza ikajitokeza siku ya uchaguzi.

"Kwenye hili naomba niwatoe hofu wananchi kwa kuwa jukumu la serikali ni kuwalinda raia na mali zao hivyo tutahakikisha utulivu unakuwepo na kama itatokea changamoto ya aina yeyote vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria  vitatimiza wajibu wake bila kuathiri misingi ya haki wala huduma zingine zinazoendelea ndani ya mkoa wa Iringa"alisema.

RC Kheri amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama pale itakapohitajika endapo patakuwa na changamoto yeyote ya kiusalama kwenye eneo lolote.

"Niwakumbushe tu kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vitatimiza wajibu huo wa kulinda usalama wa raia na mali zao kwa  kuzingatia sheria taratibu na haki za kila mmoja katika zoezi hilo la uchaguzi"

Aidha amewataka wananchi wa mkoa wa iringa kuendelea kufatilia maelekezo ya tume huru ya uchaguzi kuhusu uchaguzi kuanzia sasa hadi siku ya uchaguzi ili kupata maelekezo ya jumla, ufafanuzi wa mambo mbalimbali na kusaidia kufanya wajibu wako wa kupiga kura bila kuathiri taratibu za kisheria zilizowekwa.

Tume huru ya uchaguzi ndio chombo kilichopewa mamlaka ya kuelekeza kusimamia na kutangaza .

Alisema kuwa pamoja kwamba oktoba 29 kutakuwa na zoezi la kupiga kura anawahakikishia kuwa huduma zote za msingi ndani ya mkoa wa iringa zitakuwa zinaendelea.

Alisema kuwa maeneo ya huduma kama Hospitali, masoko na maduka huduma zitakuwa zinaendelea hivyo niwatoe mashaka kuwa pamoja na zoezi hilo lakini huduma za msingi zitakuwa zinaendelea

Maeneo ambapo huduma zitasimama ni yale maeneo ambayo ni kazi za umma kama vile ofisi za umma zote hazitafanya kazi na mashule.

"Niwahamasishe wale wote waliojiandikisha kwenda kuhakikisha taarifa zao na kufahamu vituo vyao vya kupigia kura ili baada ya hapo akatimize wajibu wake wa kwenda kuwachagua viongozi watakao tuwakilisha katika mamlaka mbalimbali zilizotamkwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ili mwisho wa siku tupate viongozi ambao watasimamia maendeleo ya mji wa Iringa"alisema

MWISHO.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI