Wananchi na wapigakura wa Tanzania wamesisitizwa kupuuza na kutokubali kuhadaika na watu na baadhi ya wanasiasa wanaohamasisha vurugu na maandamano Jumatano ya Oktoba 29, 2025 siku ya upigaji wa kura kwenye uchaguzi Mkuu wa Tanzania.
Wananchi tuliozungumza nao akiwemo Shaban Maulid na Adrian Malikale wamewasihi wananchi kujifunza na kutathmini athari za vurugu na machafuko kwa jamii hasa kwa watoto, wanawake na wazee, wakiahidi kutoandamana na kusisitiza kufuatwa kwa taratibu na sheria zinazotambulika kisheria wakati wa zoezi la upigaji kura.
"Ni muhimu sana kutokubali kushawishiwa au kudanganyika kwenda kuandamana kwa namna yoyote ile ifikapo Oktoba 29, 2025. Tujitokeze tupige kura, turudi nyumbani kuendelea na shughuli zetu kama mimi mama lishe nitakavyofanya. " amesema Bi. Zuhura Mohamed.
Tayari serikali ya Tanzania kupitia kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewahakikishia watanzania wote utulivu, amani na usalama siku hiyo ya upigaji wa kura, wakihimiza kila mmoja kujitoke kwa wingi kumchagua Kiongozi wamtakaye bila ya hofu yoyote na kubainisha kuwa wamejipanga kuhakikisha kila mmoja anaitumia haki yake ya kikatiba bila bugudha, usumbufu na hofu ya vurugu.
0 Comments