Header Ads Widget

RC SENYAMULE; "THAMANI YA ARDHI YAPAA,DODOMA SASA NI KITUO KIKUU CHA MAENDELEO NCHINI.

 



Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma


MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kuwa thamani ya ardhi katika jiji la Dodoma inaendelea kupanda kwa kasi kila siku, kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimiundombinu yanayoendelea kujitokeza katika mji huo ambao sasa ni makao makuu ya nchi.


Akizungumza jijini Dodoma katika kikao na viongozi wa dini mbalimbali, Senyamule alisema kuwa mabadiliko ya Dodoma kutoka kuwa mji mdogo hadi kuwa jiji linaloongoza kwa kasi ya ukuaji yamefungua milango ya uwekezaji, ajira, na ustawi wa wananchi kwa ujumla.


“Zamani ukisema unaishi Dodoma mtu anakushangaa, lakini leo hii Dodoma imekuwa ndoto ya kila Mtanzania. Kila mtu anatamani kuwa sehemu ya mabadiliko haya Ardhi ya Dodoma sasa ni dhahabu  thamani yake inapanda kila kukicha,” amesema Senyamule.


Aidha, amebainisha kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na wananchi kwa kuhakikisha huduma muhimu kama maji safi na salama, umeme wa uhakika, barabara za lami, pamoja na upatikanaji wa ardhi kwa taratibu halali, zinapatikana kwa urahisi.


 “Mji huu umejengwa kwa misingi ya mpango bora wa matumizi ya ardhi tuna miundombinu ya kisasa, hospitali za kisasa, shule, taasisi za elimu ya juu, na sasa tunajivunia kuwa mwenyeji wa taasisi na wizara zote za serikali kuu,” aliongeza.



Katika mazungumzo hayo na viongozi wa dini, Mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi hao kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhamasisha amani, mshikamano, na maadili mema miongoni mwa wananchi, hasa katika kipindi hiki cha ukuaji wa kasi wa jiji.


Pia, amewasihi wananchi wote wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla  kuchangamkia fursa za uwekezaji, hasa katika sekta za makazi, biashara, kilimo cha kisasa, huduma za kijamii, na utalii, akisema kuwa jiji hilo lina fursa nyingi ambazo bado hazijachukuliwa.


 “Dodoma si ya watumishi wa serikali peke yao tena hii ni fursa kwa wakulima, wafanyabiashara, wajasiriamali, vijana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi hatutaki mtu abaki nyuma,” amesisitiza.


Hata hivyo Senyamule ametoa wito kwa mamlaka za mipango miji, ardhi na uwekezaji kuhakikisha zinatoa ushirikiano wa karibu kwa kila mtu anayehitaji kujenga au kuwekeza kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI