Na Moses Ng’wat, Ileje.
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amewataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali ikiwemo barabara na madaraja, akisisitiza kuwa hatua hiyo italeta manufaa ya muda mrefu kwa Taifa.
Ametoa kauli hiyo,Oktoba 4, 2025 mara baada ya kukagua na kuzindua daraja la mawe (box culvert) lenye midomo minne lililojengwa katika barabara ya Mapogoro – Mtima, wilayani Ileje, mkoani Songwe.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa barabara ya Mapogoro – Mtima yenye urefu wa kilometa 2, ikiunganisha na ile ya Mlale – Ikumbilo yenye kilometa 14, ukitekelezwa na mkandarasi, Ngongo and Sons Construction Limited kutoka Wilayani Mbozi.
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Ileje, Mhandisi Lugano Mwambingu, ujenzi wa daraja hilo ulianza Agosti 29, 2024 na kukamilika Mei 29, 2025 kwa gharama ya Sh. 59.5 Milioni, fedha zilizotolewa kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund).
Alisema daraja limekamilika kwa asilimia 100 na tayari limeanza kutumika, likiunganisha vijiji vya Mapogoro na Mtima na kurahisisha wananchi kufikia huduma muhimu za kijamii ikiwemo shule na zahanati.
“Mbali na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, daraja hili limejengwa pia kama 'relief culvert' ili kulinda miundombinu ya barabara ambayo mara kadhaa ilikuwa ikiharibiwa na mafuriko,” alisema Mhandisi Mwambingu.
Aidha, alibainisha kuwa mradi huo pia umechangia kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wananchi, hivyo kuongeza kipato na ustawi wa jamii.
Kwa niaba ya wananchi, Mhandisi Mwambingu alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi katika sekta ya barabara, akisisitiza kuwa miradi kama hiyo inazidi kufungua fursa za kiuchumi katika wilaya ya Ileje.
Mwisho.








0 Comments