"Ukitaka kufika haraka nenda peke yako, ukitaka kufika mbali nenda na wenzio," Dame Sarah Mullally alisema katika hotuba yake ya kwanza ya umma kama Askofu Mkuu mpya wa Canterbury.
Lakini chaguo la Ijumaa - kwa mara ya kwanza kabisa - la mwanamke kama kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Anglikana na Ushirika wa Kianglikana duniani kote tayari inaonekana kama linaweza kuzidisha mpasuko mkubwa ndani ya jumuiya hiyo.
The Global Fellowship of Confessing Anglican (Gafcon), ambao ni mtandao wa makanisa ya kihafidhina ya Anglikana kote barani Afrika na Asia, walipokea habari hiyo "kwa huzuni".
Kanisa la Kusini mwa Afrika, kwa upande mwingine, liliita uteuzi huo wa "kihistoria" na kusema "tunakaribisha kwa moyo mkunjufu tangazo hilo".
Kanisa la Anglikana - ambalo baadhi ya watu huliita "Kanisa Mama" kwa sababu lilikuwa Kanisa la kwanza la Anglikana - linachukuliwa kwa mtazamo mpana kuwa lilichokuwa mwelekeo wa uhuru zaidi kuliko makanisa mengine duniani, hata Afrika, ambapo inakadiriwa kuwa theluthi mbili ya watu wake ni Waanglikana.
Masuala ambayo yanagawanya Ushirika wa Kianglikana wa kimataifa ni pamoja na kuwekwa wakfu kwa maaskofu wanawake mwaka wa 2014 na kukubalika kwa mahusiano ya jinsia moja mwaka wa 2023.
Wakristo wengi wa kihafidhina wanaamini kwamba wanaume pekee ndio wanapaswa kutawazwa kama maaskofu.
Katika taarifa yake Mchungaji Dk Laurent Mbanda, Askofu Mkuu wa Rwanda na mwenyekiti wa baraza la uongozi la Gafcon, alitoa hoja kwamba "wengi wa Ushirika wa Anglikana bado wanaamini kwamba Biblia inahitaji uaskofu wa wanaume pekee".
Gafcon pia ilipinga Dame Sarah kuunga mkono kubarikiwa kwa wapenzi wa jinsia moja, wakimtuhumu kwa kuendeleza "mafundisho yasiyo ya kibiblia na kufanya mabadiliko katika ndoa na maadili ya ngono".
Gafcon ilianzishwa mwaka wa 2008 kukabiliana na tofauti za kitheolojia ndani ya Ushirika wa Kianglikana, hasa kuhusu suala la ndoa za watu wa jinsia moja.
Wakati huo walitoa taarifa ambayo iliwataka viongozi wa makanisa ambao walikuwa wamepotoka kutoka kwa kile walichokiita "miongozo ya Orthodox" kutubu.
Ingawa walikuwa wazi kwamba hawakujitenga na Ushirika wa Kianglikana, walikataa wazo kwamba "kitambulisho cha Anglikana ni lazima kuamuliwa kupitia kutambuliwa na Askofu Mkuu wa Canterbury".
Mgawanyiko huo uliongezeka mnamo mwaka 2023, wakati kikundi hicho kilikataa uongozi wa Askofu Mkuu wa zamani wa Canterbury, Justin Welby, juu ya mapendekezo ya kubariki wapenzi wa jinsia moja, na hivyo kuongeza hofu ya mgawanyiko katika Kanisa.
Gafcon inadai kuongea kwa niaba ya Waanglikana wengi duniani, ingawa hilo linapingwa, na mtazamo kote barani Afrika kwa vyovyote vile sio wa kutegemea kanuni moja.
Askofu Mkuu wa Cape Town, Thabo Makgoba, ambaye anaongoza Kanisa la Kusini mwa Afrika alitaja uteuzi wa Dame Sarah "maendeleo ya kusisimua".
Ingawa Afrika Kusini inachukuliwa kuwa ya kimaendeleo zaidi kuliko nchi nyingine katika suala la mtazamo wake, tangazo hilo pia lilikaribishwa kwengineko.
Askofu Emily Onyango - mwanamke wa kwanza kutawazwa kuwa askofu katika Kanisa la Kianglikana la Kenya - alizitaja habari kwamba Dame Sarah ametajwa kuwa Askofu Mkuu kuwa "Mwamko upya".
Aliiambia BBC Focus on Africa kwamba maoni ya Gafcon si ya kitheolojia wala ya kibiblia, lakini zaidi "ya mfumo dume, ambayo hayana manufaa sana kwa Kanisa".
Askofu Onyango alisema askofu mkuu mpya alikuwa "mtu mnyenyekevu [ambaye] anasikiliza, jambo ambalo Kanisa linahitaji.
"Unapokuwa na msimamo mkali na usiwasikilize watu, hapo kuna matatizo mengi.
"Askofu mkuu mpya anatakiwa kushughulikia amani katika bara hili. Wanawake na watoto wanateseka, na anahitaji kufanya kazi kwa ajili ya amani na upatanisho."
Hilo linamweka Askofu Onyango katika migogoro na askofu mkuu wa nchi yake, ambaye ni sehemu ya uongozi wa Gafcon.
Askofu Mkuu wa Rwanda alipoulizwa kama wakati huu unaweza kuthibitisha kuwa mpasuko usioweza kurekebishwa katika Ushirika wa Anglikana duniani kote, alituma ujumbe uliosema kwamba "hakuna jambo lisiloweza kurekebishwa kwa Mungu, lakini linahitaji toba.
"Gafcon daima imekuwa ikitoa wito kwa viongozi wa kanisa waliokosea kutubu na kurudi kwenye mafundisho ya Biblia. Lakini hadi wafanye hivyo, hatuwezi kutembea nao katika ukengeufu wao."
MWISHO.
0 Comments