Na Matukio Daima Media
SERIKALI imeipongeza Shule ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam kutokana na mafanikio ya kitaaluma na mchango wake kwa serikali katika sekya ya elimu.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mdhibiti Ubora wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Albert Mutalemwa wakati wa mahafali ya shule ya Awali na Msingi Hazina jijini Dar es Salaam.
Alisema ameshangazwa na namna wanafunzi wa shule hiyo walivyomudu kutafsiri kwa vitendo mtaala wa elimu na elimu ya amali kwa ,kuonyesha vipaji vya hali ya juu kwenye michezo mbalimbali ikiwemo sarakasi.
Aliutaka uongozi wa shule hiyo kuendelea kulea vipaji na kuvumbua vipaji mbalimbali vya watoto kwani vitakuwa na msaada kwao kwa siku zijazo.
Alisema kiwango kikubwa cha maarifa walichoonyesha wanafunzi wa shule hiyo kwenye maonyesho mbalimbali ya kitaaluma kinadhihirisha elimu bora inayotolewa na shule hiyo.
Alisema wanafunzi hao wameonyesha umahiri wa hali ya juu kuelezea masuala mbalimbali yakiwemo ya sayansi na tiba ya magonjwa mbalimbali kana kwamba ni madaktari.
“Walimu kwa upande wao wanafundisha vizuri sana na mmeona namna gani watoto wameelezea kwa umahiri wa hali ya juu hapa lakini wazazi mnapokuwa nyumbani hakikisheni watoto wanakuwa na maadili mema na waepuke kukaa na makundi yanayoweza kuwasababishia kupata tabia za ovyo,” alisema
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Omari Juma aliwashukuru wazazi kwa kuwaamini na kuwapa watoto wao wawafundishe na aliahidi kuwa wataendelea kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kwenye mtihani ya kitaifa.
“Tumekuwa tukifanya vizuri sana na kushika nafasi ya kwanza kwenye mitihani kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kitaifa lakini nawahakikishia wazazi hatutabweteka na badala yake tutahakikisha tunabaki kwenye ubora ule ule,” alisema
“Wanafunzi wa Hazina wamefundishwa kujiamini na kuzungumza kwa lugha ya Kingereza kwa ufasaha mbele za watu na ndiyo sababu mwaka jana walichaguliwa kwenda kwenye siku ya Umoja wa Mataifa, walizungumza na walikonga nyoyo za wageni waalikwa,” alisema
Mwisho
0 Comments