Na Matukio Daima Media
TAASISI za kidini na kielimu kwa kushirikiana na Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Iran zimefanya mdahalo maalumu Jijini Dar Es Salaam wenye lengo la kusisitiza na kudumisha amani, mshikamano, utulivu na haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.
Mdahalo huo umewakutanisha viongozi wa dini, wanazuoni, na wadau wa amani ambapo Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelical Fellowship Church Tanzania, Baba Askofu Charles Asher, amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia haki yao ya kikatiba kwa amani katika kuchagua viongozi wanaowataka, huku akisisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuwa mfano wa utulivu barani Afrika tangu ilipopata uhuru.
Amesema uchaguzi siyo uwanja wa uhasama, bali ni fursa ya kuimarisha demokrasia na kujenga mustakabali wa taifa. “Kila mmoja wetu ana jukumu la kulinda amani. Tofauti za kisiasa haziwezi kuwa sababu ya kuvuruga umoja tuliojenga kwa miaka mingi,” amenukuliwa akisema Askofu Asher.
Kwa kadri teknolojia inavyozidi kukua na kadri uhuru unavyoongezeka wakati mwingine kumekuwa na hali za taharuki kwasababu ya kutokuwa na mwelekeo mmoja wa watu na sisi kama Viongozi wa dini ni kuileta jamii pamoja na kuwafundisha namna ya kuyapokea yaliyo mema. Tunawajibika pia kuwaweka pamoja na kutunza tunu ya umoja wa Watanzania." Amesema Askofu Asher.
0 Comments