Na Josea Sinkala, Mbeya.
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kupata nafasi mbalimbali za kujifunza na kujiajiri.
Kauli hiyo imeelezwa na Katibu Mtendaji wa NACTVET Dkt. Mwajuma Lingwanda, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa mkoani Mbeya.
Bi. Lingwanda amesema, vijana wana nafasi ya kujitokeza na kujiunga na vyuo vya ufundi, elimu za amali na masuala mbalimbali ya ufundi ili kujiajiri katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utolewaji elimu ikiwemo ufundi na ufundi stadi hivyo vijana mbalimbali bila kujali kiwango cha elimu wana nafasi ya kwenda kujiunga na vyuo vya ufundi ili kujifunza masuala ya ufundi.
Kiongozi huyo amesema NACTVET imeshiriki maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa ili kuendelea kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali nchini na kuwaonyesha fursa zilizopo.
0 Comments