Na mwandishi wetu
Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini pamoja na waandishi wa habari, wametakiwa kutumia nafasi zao kwenye jamii kuhimiza amani na umoja wa kitaifa, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu, ili kuepusha mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa Mkoani Iringa leo Alhamisi Oktoba 09, 2025 wakati wa warsha ya siku moja iliyoratibiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikisha waandishi wa habari na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali Mkoani humo.
Mwezeshaji wa semina hiyo, Uzima Justine, amesema huu ni wakati sahihi kwa viongozi wa dini kutoa ujumbe unaowaunganisha Watanzania, badala ya maneno yanayoweza kuchochea chuki au migawanyiko.
“Chochote kisichounganisha watu na kuleta amani si cha kweli,” alisema Uzima, akisisitiza kwamba wajibu wa viongozi wa dini ni kujenga maridhiano na upendo wakati wote, hasa katika kipindi cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Mratibu wa warsha hiyo, Omary Ibrahim, ambaye ni Afisa Miradi wa BAKWATA Makao Makuu, alisema warsha hiyo imelenga kuwaongezea uelewa washiriki kuhusu nafasi yao muhimu katika kulinda amani kupitia maneno na matendo yao.
“Tupo Iringa na tumewakutanisha waandishi wa habari pamoja na viongozi wa dini — watu ambao wanaweza kujenga au kubomoa. Lengo letu ni kuwajengea uwezo ili wakatoe elimu sahihi kwa wananchi, wasitoke nje ya misingi ya ukweli,” alisema Omary.
Aliongeza kuwa wakati mwingine haki ya kukusanya, kuchakata na kusambaza habari haitumiki ipasavyo, jambo linaloweza kuleta mkanganyiko kwa jamii na kuhatarisha amani ya nchi.
Katika warsha hiyo wito umetolewa kwa taasisi za dini na vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu zaidi katika kutoa elimu ya uraia, kueleza kwa uwazi umuhimu wa amani, na kupinga taarifa au mafundisho yanayoweza kugawa jamii.
0 Comments