Na,Jusline Marco;Arusha
Mradi wa maji unaotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro unatarajia kuwanufaisha wananchi wa Kata za Endulen,Alaetoli na Kakrsio zilizopo katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambapo kwa kata ya Endulen eneo la Mlima Matiti kimechimbwa kisima chenye urefu wa mita 250 chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita za maji 80,000 kwa siku.
Akikagua ujenzi wa mradi huo ambao utekelezaji wake upo zaidi ya asilimia 50, ikiwa ni ziara yake ya kikazi Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia wananchi wa kata hizo na baadae Olbalbal kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji kwa mifugo hasa msimu wa kiangazi.
"Baada utafiti atika Kata hii ya Endulen tumepata maji ya kutosha, kisima kilichochimbwa katika eneo hili kitazalisha lita 80,000 kwa saa na lita laki moja (100,000) kwa siku, tunaamini ndani ya wiki moja majaribio ya mwisho ya kujaza maji yatakuwa yamekamilika, mabwawa ya kukusanya maji yatachimbwa na mifugo zaidi ya 2000 itakuwa inapata maji hapa kila siku,” alifafanua Badru
Kamishna Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa ajili ya wananchi wanaoishi eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kijamii ambayo wananchi waliomba Mamlaka hiyo kuwasaidia ili kukabiliana na changamoto za ukame na kuepuka kuingiza mifugo maeneo maalum ambayo hayaruhusiwi kuingiza mifugo ndani ya hifadhi.
Baada ya kukamilika mradi wa maji katika kata ya Endulen, visima vingine vitachimbwa katika kata za Kakesio na Olbalbal ambapo wananchi watanufaika kwa kuweza kunywesha mifugo yao pamoja na matumizi ya Nyumba.
Naye Mmoja wa wananchi wa Kata ya Endulen Siyapaa Ole-Keyan amesema utekelezaji wa miradi katika kata hizo Serikali imejibu kilio cha kunusuru mifugo yao hasa kipindi cha kiangazi na wao kujiepusha kupeleka mifugo yao maeneo yasiyoruhusiwa katika nyanda za misitu na eneo la Ndutu ambalo ni mazalia ya Nyumbu wanaohama.
0 Comments