Na Chausiku Said
Matukio Daima Mwanza
Viongozi wa dini ya kiislamu na wakristo Mkoani Mwanza wameungana kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi.
Wito huo umetolewa kupitia Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, katika kongamano la amani lililowakutanisha viongozi wa dini mbalimbali na serikali, likiwa na lengo la kuhimiza umoja, utulivu na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, pamoja na Askofu Dk. Charles Sekelwa, walisema viongozi wa dini wataendelea kushirikiana na serikali kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa uhuru na kwa amani.
“Sisi kama Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza tutaendelea kuhamasisha wananchi wa mkoa huu na nchi nzima kujitokeza kupiga kura kwa haki na utulivu. Tutaliombea Taifa letu Mungu atujalie hekima, umoja na amani katika kipindi chote cha uchaguzi,” walisema viongozi hao kwa pamoja.
Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na kuwaombea viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Hatuwezi kumuombea kiongozi au jirani kama hatumpendi. Umoja wetu ni dhahabu; tusipoutunza, hakuna atakayetuletea mwingine. Viongozi wa dini tuwahimize waumini na vijana wetu wajitokeze kupiga kura kwa amani,” alisema Nyalandu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari na serikali ipo tayari kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
“Nataka niwahakikishie viongozi wa dini, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwamba Mwanza ipo salama. Serikali inatimiza wajibu wa kulinda raia na mali zao, hivyo wananchi wajitokeze kupiga kura bila hofu,” alisema Mtanda.
0 Comments