NA MATUKIO DAIMA MEDIA,MVOMERO
TUKIO la kuchomwa moto magari mawili wilayani Mvomero limezua mjadala mpana baada ya kuibuka kwa madai yanayokinzana kuhusu kifo cha mfanyakazi wa ndani, Mwanahasan Juma Hamis (18)aliyekuwa akifanya kazi jijini Dar es salaam nyumbani Kwa familia ya Miraji Chomoka.
Tukio hilo lilmehusisha magari mawili aina ya Mazda CX-5 yenye namba za usajili T.214 EJU na Toyota Noah T.350 DCH ambayo yalichomwa moto na wananchi waliodaiwa kuwa na hasira kutokana na kifo cha mfanyakazi huyo wa ndani anayedaiwa kufanya kazi jijini Dar es salaam kwa takribani miezi nane.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, marehemu alikuwa akisafirishwa kwa ajili ya mazishi huko nyumbani kwao wilayani Mvomero Desemba 17, 2025, kabla ya wananchi kuchoma moto magari yaliyokuwa swali yamebeba waombolezaji kutokea Jijini Dar es salaam na Morogoro yakimsindikiza.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa marehemu wanadai kulikuwa na mazingira ya kutatanisha juu ya mwili wa marehemu, wakieleza kuwa walipolazimisha kuutambua walibaini hali isiyo ya kawaida, jambo lililozua hasira kwa wananchi.
Lakini taarifa nyingine zinapinga madai hayo, zikieleza kuwa mwili huo ulikuwa umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kuwekwa dawa maalumu, hatua ambayo huathiri kidogo mwonekano wa mwili.
Sintofahamu hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kuwavamia watu waliokuwa wakisindikiza Mwili kwenda nyumbani kwao kwa maziko na kusababisha vurugu ambapo licha ya watu kuokolewa na kufichwa kuepuka madhara zaidi, magari waliyokuwa nayo yaliteketezwa kwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama katika taarifa yake amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa madai hayo huku akionya dhidi ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.






0 Comments