Header Ads Widget

Makala:Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na Changamoto ya Nishati Chafu Nchini Tanzania


Na Francis Godwin ,Matukio Daima Media  

Matumizi ya nishati ya kuni na mkaa, maarufu kama nishati chafu ya kupikia, yamekuwa changamoto kubwa nchini Tanzania. 

Serikali na wadau mbalimbali duniani wanahimiza matumizi ya nishati safi kwa lengo la kuboresha afya, kulinda mazingira, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.


Angelina Kadinde, mjasiriamali wa kuni kutoka Iringa, anakiri kutokuwa na uelewa wa nishati safi, jambo linaloonyesha changamoto ya elimu kwa jamii kuhusu mbadala wa nishati chafu.

Changamoto za Upatikanaji wa Nishati Safi
Watumiaji wengine wanaona changamoto ya gharama kama kikwazo kikuu cha kuhamia nishati safi.
msamaria mwema akimsaidia Angelina Kandinde kumtwisha mzigo wa kuni.

 Bitrisi Shabani, mmoja wa wakazi wa Miyomboni katikati ya mji wa Iringa, anasema gharama kubwa za kujaza mitungi ya gesi zimemlazimu kurudi kutumia kuni.

 Hali hii pia imeathiri biashara ya majiko ya gesi, kama anavyosema Tadei Sanga, mfanyabiashara wa majiko ya gesi mjini Iringa, kwamba wateja wengi wanaotumia majiko hayo ni wanafunzi wa vyuo, huku wananchi wa kipato cha chini wakishindwa kumudu gharama.

Viongozi wa dini pia wameshauri serikali kuhakikisha bei za gesi zinashuka ili kila mwananchi aweze kumudu.

 Wameongeza kuwa matumizi ya kuni na ukataji miti kiholela vinakiuka maadili ya kidini na kuhatarisha mazingira, hali inayohitaji hatua madhubuti za upandaji miti ili kurejesha uoto wa asili.

Hatua za Kulinda Mazingira
Manispaa ya Iringa imeanzisha kampeni ya kupanda miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mchungaji wa kanisa la kiinjili la Kilutheri Afrika mashariki (KKKAM) Titus Kiungo mbali ya kupongeza serikali kwa mkakati wa kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia Bado anashauri bei ya Nishati hiyo iwe rafiki kwa Kila mmoja ili matumizi yaongezeke zaidi .

mkazi wa Miyomboni Iringa Britis Shabani akipika kupitia jiko la gesi

Kuwa changamoto kubwa ni gharama ya ujazaji gesi baada ya Kuishi mtanzania wa kipato Cha chini hawezi kumudu bei hiyo .

Leo unapozungumzia gharama ya tsh 10,000 ama 20,000 kujaza gesi kwa mtu wa mjini mwenye kipato si tatizo ila Mwananchi wa Kijijini ambae kwake 1000 ni shida kupata ataona heri kutumia muda kwenda Porini kutafuta Kuni ambazo ni za bure .

 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwanda, amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni njia mojawapo ya kukabiliana na ongezeko la joto katika mkoa huo.

Matumizi ya nishati safi si tu yanaboresha afya bali pia huokoa muda wa kupika na kuboresha hali ya maisha. 

Ni wazi kuwa umuhimu wa Nishati Safi ya Kupikia agenda ya matumizi ya nishati safi imepewa kipaumbele kimataifa kutokana na athari za kiafya na mazingira zinazosababishwa na nishati chafu. 

Mwongozo wa Benki ya Dunia wa mwaka 2020 unasisitiza kuwa nishati safi hupimwa kwa vigezo kama ufanisi, usalama, urahisi wa matumizi, unafuu wa gharama, na kiwango kidogo cha sumu. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapima teknolojia safi kulingana na kiwango cha hewa hatarishi kama kaboni monoksidi na chembechembe za vumbi zinazotolewa wakati wa kupikia.

Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi 2024-2034
Tanzania imeanzisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034, ukilenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipouzindua mkakati huu, alieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkakati huu pia umepokewa vyema na taasisi mbalimbali kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na wanasiasa. 

Wadau hawa wamejitolea kutoa elimu na kusaidia kaya zenye uhitaji kupata majiko ya nishati safi.

Aina za Nishati Zinazotumika Nchini
Nchini Tanzania, aina za nishati za kupikia ni pamoja na kuni, mkaa, mafuta ya taa, bayogesi, bayoethanol, gesi asilia, LPG, umeme, majiko banifu, na majiko yanayotumia nishati ya jua.

 Hata hivyo, kulingana na ripoti ya Cooking Energy Action Plan ya mwaka 2022, asilimia 90 ya kaya nchini bado zinategemea kuni na mkaa, ambapo kuni hutumika kwa asilimia 63.5 na mkaa kwa asilimia 26.2.

Athari za Kiafya na Mazingira
Matumizi ya nishati chafu yameleta changamoto nyingi kiafya. 

Takwimu zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 30,000 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na matumizi ya nishati chafu, huku wanawake na watoto wakiwa waathirika wakuu. 

Ni ukweli kuwa  kwa kutumia nishati safi, mtu anaweza kupunguza muda wa kupika kutoka saa saba kwa wiki hadi saa moja.

Mkakati huu wa nishati safi, elimu na upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu vinapaswa kupewa kipaumbele.

 Hivyo Serikali, wadau wa maendeleo, na wananchi wanapaswa kushirikiana kuhakikisha mabadiliko ya kudumu na endelevu yanafikiwa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI