NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime leo Jumapili Oktoba 26, 2025 amesisitiza kuwa atakayethubutu kuvunja sheria Oktoba 29, 2025 siku ya Upigaji kura nchini Tanzania kwenye uchaguzi Mkuu asilaumu kwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria kwani elimu imetolewa vya kutosha na kwa muda mrefu kupitia njia mbalimbali.
Misime ametoa kauli hiyo katika Taarifa ya Jeshi la Polisi kwa Vyombo vya habari hii leo siku mbili kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akiwahakikishia wananchi wote wa Tanzania amani na usalama wa kutosha, akiwasihi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua Viongozi wanaowataka bila ya wasiwasi na hofu yoyote.
"Tunawahakikishia kuwa tumejipanga vizuri sana kumdhibiti yeyote yule kwa mujibu wa sheria atakayejitokeza ama kwa makusudi au nia ovu kuvunja sheria za nchi ili kuhatarisha amani ya nchi kwa kisingizio chochote kile siku hiyo ya kupiga kura na baada ya kupiga kura. Atakayevunja sheria asilaumu kwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria." Amesema.
Jeshi hilo la Polisi pia limewahakikishia wageni wote wanaofika na waliopo nchini kuwa hali ya ulinzi na usalama ni shwari na hakuna tishio lolote la usalama linaloweza kufanya shughuli ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kutofanyika kwa amani wakati wa kuchagua Mbunge, Diwani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi ambao hufanyika kila baada ya kipindi cha miaka mitano.
MWISHO.






0 Comments