Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS KUPITIA CCM DKT, SAMIA SULUHU HASSAN KUFUNGA KAMPENI ZAKE RASMI OKTOBA 28 JIJINI MWANZA.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufunga rasmi kampeni zake za uchaguzi mwaka huu mkoani Mwanza, ambapo mgombea urais kupitia chama hicho, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa kihistoria katika Viwanja vya CCM Kirumba, Oktoba 28, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuhitimisha kampeni za chama hicho, pia kutoa fursa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa kuzungumziwa masuala muhimu yanayohusu maendeleo yao.

"Chama chetu kimefanya kazi kubwa kutoka kuanzishwa kwake hadi leo, na tunapomaliza kampeni hizi, tunataka kuonesha mafanikio yaliyofikiwa, hasa katika Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Mwanza," alisema Mtuwa.

Aliongeza kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tangu aingie madarakani, amefanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, na miundombinu, na mkutano huo utakuwa ni nafasi nzuri ya kumshukuru kwa jitihada hizo.

"Rais wetu amefanya mengi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, na lengo letu ni kuwakaribisha wananchi wote kuja kushiriki katika ufungaji wa kampeni na  tutakuwa na mkutano wa kisayansi utakaoshirikisha wananchi, na tunategemea kuwa utakuwa wa amani na utulivu," alieleza Katibu huyo.

Mtuwa alisisitiza kuwa Mkoa wa Mwanza ni muhimu kwa chama hicho kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura, ambapo takribani milioni 2 wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi. Aliongeza kuwa CCM inatumia kila fursa kuhakikisha inapata ridhaa ya wananchi ili kuendelea kuleta maendeleo katika maeneo hayo.

"Tunajivunia kuwa Mkoa wa Mwanza ni kitovu cha Kanda ya Ziwa. Tuna idadi kubwa ya wapiga kura, na kama chama, tunawajibika kufanya kampeni za kistaarabu, na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu sera zetu na maendeleo tunayoyatekeleza," alisisitiza Mtuwa.

Aidha amefafanua kuwa  mkutano huo utakuwa wa amani, na chama kimejipanga kuhakikisha usalama na ulinzi wa wananchi unaimarishwa. Aidha, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kumaliza kampeni hizo kwa kishindo.

"Serikali ya CCM imejipanga kulinda usalama wa wananchi kutoka mwanzo wa kampeni hadi siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025," aliongeza.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI