Rais wa Marekani Donald Trump ametoa taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social unaoonyesha kuwa Hamas imekubali mpango wa amani.
Ujumbe wa Trump unasema: "Kulingana na Taarifa iliyotolewa hivi punde na Hamas, ninaamini wako tayari kwa AMANI ya kudumu. Israel lazima isitishe mara moja mashambulizi ya mabomu huko Gaza, ili tuweze kupata mateka kwa usalama na haraka!
"Kwa sasa, ni hatari sana kufanya hivyo. Tayari tuko kwenye majadiliano kuhusu maelezo yatakayofanyiwa kazi. Hili halihusu Gaza pekee, hili ni kuhusu AMANI iliyotafutwa kwa muda mrefu katika Mashariki ya Kati."
Hamas wamesema nini?
Katika taarifa yake ikijibu pendekezo la amani la Marekani, Hamas inasema inakubali "kuwaachilia wafungwa wote wa Israel, walio hai na waliokufa, kwa mujibu wa mpango wa mabadilishano uliopendekezwa na Rais Trump, mradi masharti ya ubadilishanaji yametimizwa".
Taarifa hiyo inaongeza kuwa "inafanya upya makubaliano yake ya kukabidhi utawala wa Ukanda wa Gaza kwa chombo huru cha Wapalestina" kwa kuzingatia "makubaliano ya kitaifa ya Palestina na uungaji mkono wa nchi za Kiarabu na Kiislamu".
Juu ya mustakabali wa Gaza na haki za watu wa Palestina, Hamas inasema hii "inahusishwa na msimamo wa kitaifa unaozingatia sheria na maazimio husika ya kimataifa, na inajadiliwa ndani ya mfumo wa kitaifa" ambao itakuwa sehemu yake.
0 Comments