Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB), imeanza kuchakata na kusambaza tani 28,000 za mbegu ikiwa ni maandalizi ya msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026, huku ikiwaondoa hofu wakulima wa zao hilo juu ya upatikani wa Mbegu za kupanda na kuahidi kuwa kila mkulima atafikiwa na Pembejeo hiyo muhimu kabla ya kuanza kulima.
Aidha, Bodi hiyo imsema kuwa imzalisha mbegu za kutosha katika msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026 na kuwataka wakulima kuendelea kufanya maandalizi ya mashamba ikiwemo kukata, kung'oa na kuondoa masalia ili kudhibiti uhamaji wa Wadudu kutoka msimu mmoja kwenda mwingine ambao wanashambulia zao hilo la kimkakati nchini.
Msimamizi wa uchakataji wa Mbegu kutoka Bodi ya Pamba, Ndinda Anthony ambaye pia ni Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Bariadi, amesema kuwa mbegu ya msimu huo inatolewa na serikali kupitia Bodi ya Pamba na kwamba wanatarajia kuchakata kiasi cha mbegu Tani elfu 15.
Amesema zoezi la upokeaji wa mbegu litafungwa wiki hii na kubakiza zoezi la uchakataji wa Mbegu ambapo hadi sasa wamechakata mbegu tani elfu 7.8 ambapo mbegu hizo zimeshaanza kupelekwa kwa Wakulima wa pamba katika wilaya mbalimbali.
"Kiwanda Cha Triwin kitasambaza mbegu za Pamba Kwa wakulima wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara pia kutokana na mahitaji, mbegu hiyo itasambazwa Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine...mbegu ya msimu huu imezingatia ubora unaohitajika yaani uoataji" amesema Ndinda.
Amesema kuwa endapo mkulima akipata mbegu yenye Ubora ni moja ya sifa ya kujihakikishia mavuno na kwani mavuno ya Pamba yanaanzia kwenye ubora wa mbegu ambapo kila mbegu inayoandaliwa na Bodi ya Pamba ili kwenda kwa Wakulima inafanyiwa majaribio.
Amewataka wakulima wa Pamba katika msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026 kuondoa wasiwasi kwani inayoandaliwa katika msimu huu inatoa kwa zaidi ya asilimia 98.
"Wakulima wa pamba wasiwe na wasiwasi mbegu ya mwaka huu inatoa, serikali iko bega kwa bega na wakulima kuhakikisha kusudi la kuzalisha kwa tija linafikiwa...Wilaya za Mkoa wa Simiyu zimeshapata mbegu na tunaongeza mbegu kulingana na mahitaji na molali wa wakulima na serikali itahakikisha kila mkulima anayelima Pamba anapata mbegu" amesema.
Ameongeza kuwa mahitaji ya mbegu za Pamba nchi nzima ni tani elfu 28,000, huku Mkoa wa Simiyu ambao ni kinara wa uzalishaji wa pamba unahitaji mbegu Tani elfu 14 na kwamba Bodi ya Pamba imeandaa mbegu za kutosha kukabiliana na upungufu wowote ambao unaweza kujitokeza.
Mwisho.
0 Comments