Header Ads Widget

SH MILIONI 600 KUJENGA SOKO LA MADINI MKWAJUNI.

 

Na Moses Ng’wat, Songwe.

Zaidi ya Sh milioni 600 zinatarajiwa kutumika kujenga soko jipya la madini katika mji wa Mkwajuni, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, mradi unaolenga kuboresha biashara ya madini na kuongeza mapato ya halmashauri.

Mradi huo wenye vibanda 40 umewekwa jiwe la msingi  Oktoba 6, 2025 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Songwe, Cecilia Kavishe, Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Songwe, Maria Chacha, alisema mradi unatekelezwa na mkandarasi Okasseny Engineering Limited kwa awamu mbili kwa gharama ya Sh milioni 600.

Katika awamu ya kwanza Sh milioni 389.6 zimetolewa na kati yake Sh milioni 187.9 zimetumika kujenga miundombinu ya jengo lenye vyumba 40, eneo la kusubiria, vyoo sita na sehemu ya usahihi wa madini.

Hata hivyo, alisema ujenzi huo umekumbwa na changamoto za upatikanaji wa umeme na maji hali iliyosababisha kushindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa wa Septemba 13, 2025.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, alisema soko hilo litasaidia halmashauri kuongeza mapato kupitia ushuru wa madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.

“Sekta ya madini inalipatia taifa pato kubwa linalotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na maji. Nawasihi wafanyabiashara mlitunze na mlitumie ipasavyo soko hili kwa maendeleo ya sekta ya madini na kulipa kodi stahiki,” alisema Ussi.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Songwe, Chone Malembo, alisema soko jipya litakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya maeneo duni ya kuuzia madini.

Alisema kwa sasa soko linalotumika lina vyumba 26 pekee wakati uhitaji ni zaidi ya vibanda 50, hivyo kukamilika kwa mradi mpya kutapunguza tatizo hilo na kurahisisha shughuli za biashara ya madini mkoani humo.
Mwenge wa  uhuru unatarajiwa kukabidhiwa Mkoani Mbeya kesho, Oktoba 7 2025 baada ya kukimbizwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI