Na Shemsa Mussa -Matukio Daima
Messenyi,Kagera.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanzisha mpango imilifu wa mfumo wa chakula unaolenga kuwawezesha wakulima nchini, hususan wa maeneo ya vijijini, kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi na ziada kwa ajili ya kuuza ili kuinua uchumi wao kupitia kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumza katika kijiji cha Kilimilile, kata Kenyana, wilayani Missenyi, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye pia ni Mratibu wa Mfumo Himilivu wa Chakula, Timotheo David Semuguruka, alisema Serikali imejipanga kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo kwa kuweka msukumo mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Semuguruka alisema Wizara ya Kilimo imejikita katika kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo kwa kuchimba visima, kujenga mabwawa na skimu za umwagiliaji ili wakulima waweze kulima mara mbili kwa mwaka na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato.
“Lengo letu ni kuona wakulima wanapata chakula cha kutosha na kipato kupitia kilimo chenye tija. Hii itasaidia kufikia malengo ya Taifa ya usalama wa chakula,” alisema Semuguruka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Khamis Maiga, amewataka wakulima wa kijiji cha Kilimilile kuweka mikakati madhubuti ya kilimo ili kuongeza tija na kuhakikisha uzalishaji unakuwa endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjati Fatma Mwassa, alisema kuwa mradi wa umwagiliaji ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata chakula cha kutosha na kuongeza uzalishaji wa kilimo cha kibiashara.
“Mradi huu unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 300, na utawasaidia wakulima wadogo kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na kujiongezea kipato,” alisema Mwassa.
Aidha, Mwassa aliwataka wakulima wa kata hiyo kujisajili kwa wingi ili waweze kunufaika na ruzuku ya mbolea kwa bei nafuu itakayowawezesha kupiga hatua zaidi katika kilimo chenye tija.Kwa mujibu wa maelezo ya Wizara ya Kilimo, jumla ya skimu 58 za umwagiliaji zimepelekwa mkoani Kagera kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogowadogo kulima kwa tija. Kati ya hizo, 15 zitatolewa Missenyi, 15 Bukoba Vijijini, huku Muleba na Ngara zikipewa skimu 28
Jumla ya wakulima 638 kutoka wilaya za Muleba, Missenyi, Ngara na Bukoba Vijijini wanatarajiwa kunufaika na mpango huo. Maafisa ugani wametakiwa kuhakikisha mashamba yanaandaliwa vizuri, mbegu bora zinapandwa, na matumizi sahihi ya mbolea yanafuatwa ili kuongeza uzalishaji kupitia programu hiyo ya umwagiliaji.



.jpeg)
.jpeg)




0 Comments