Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehitimisha rasmi kampeni za CCM Zanzibar na kutangaza sekta 11 za kipaumbele atakazozipa msukumo katika awamu ijayo ya uongozi wake.
Akizungumza leo, tarehe 26 Oktoba 2025, katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inayoongozwa na CCM itaendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa wananchi kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa wote.
Amefafanua kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu inayoendelea, Serikali ijayo itaendeleza miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo bandari, barabara na viwanja vya ndege, hususan Uwanja wa Ndege wa Pemba, Bandari za Mangapwani na Fumba, na kuimarisha zaidi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Aidha, ujenzi wa barabara kuu kama ya Tunguu–Makunduchi na madaraja ya Chwaka na Charawe utapewa kipaumbele, kwa lengo la kuunganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.
Katika sekta ya elimu, Serikali itaendelea kujenga skuli za ghorofa za msingi na sekondari katika wilaya zote, wakati katika sekta ya afya, Dkt. Mwinyi ameahidi kujenga Hospitali kubwa ya Saratani Binguni, kuendeleza Hospitali ya Mnazi Mmoja, pamoja na Hospitali ya Rufaa na Kufundishia Binguni.
Kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama, Dkt. Mwinyi amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 55 kwa miradi ya maji katika Mikoa ya Kusini Unguja na Mjini Magharibi, ikiwemo ujenzi wa matangi makubwa yenye ujazo wa lita milioni moja.
Katika sekta ya ajira, amesema Serikali itazalisha zaidi ya ajira 350,000, kupitia ajira za umma, sekta binafsi, na programu za kuwezesha vijana kujiajiri wenyewe.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba kwa wakulima wa mwani na wajasiriamali wadogo.
Akizungumzia usalama wa chakula, Dkt. Mwinyi ameahidi kujenga maghala ya chakula kwa ajili ya kuhifadhi akiba na kudhibiti mfumuko wa bei, huku kwenye sekta ya kilimo akiahidi kuwapatia wakulima mbegu bora, pembejeo, mafunzo na mikopo nafuu.
Pia, amesema Serikali itawekeza katika nishati ya mafuta kwa kujenga matangi makubwa ya kuhifadhia petroli, ili kudhibiti changamoto za upatikanaji na mabadiliko ya bei.
Kwa upande wa makazi, Dkt. Mwinyi ameahidi kuendeleza ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu, pamoja na kuanzisha mji wa kisasa wa michezo utakaokwenda sambamba na ujenzi wa Uwanja wa AFCON.
Amehitimisha kwa kusema kuwa Serikali itazingatia ongezeko la mishahara na pensheni kwa wastaafu kadri uchumi unavyozidi kukua, na kuwaomba wananchi wamchague tena kwa kura nyingi ili aendelee kuiongoza Zanzibar katika awamu inayofuata.




















0 Comments