Header Ads Widget

MWENYEKITI CCM MKOA WA IRINGA DAUD YASSIN AOMBA KURA ZA MBUNGE KIHENZILE ,RAIS DKT SAMIA NA MADIWANI CCM OKTOBA 29

Na Matukio Daima Media, Mufindi

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na mchakato wa uchaguzi unaofanyika nchini, akibainisha kuwa ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si kwa matakwa ya chama chochote.

Huku akiomba kura za kutosha kwa Dkt Samia Suluhu Hassan ,mgombea ubunge Mufindi Kusini David Kihenzile na madiwani wote wa CCM.


Yassin ametoa kauli hiyo leo   wakati akihitimisha kampeni katika Jimbo la Mufindi Kusini, kwenye mkutano uliofanyika katika Kata ya Malangali, ambapo amesisitiza wananchi kupuuza propaganda za upotoshaji zinazoenezwa mtandaoni.

 “Uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa Katiba, na kila baada ya miaka mitano wananchi huchagua Rais, Wabunge na Madiwani. Hakuna jambo lililokiukwa wala kupindishwa,” alisema Yassin.

Ameongeza kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametahadharisha kuwa hakutakuwa na vurugu wala changamoto za kiusalama, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 na kurejea makwao kusubiri matokeo kwa utulivu.

Aidha, Yassin amewahakikishia wakazi wa Iringa kuwa hali ya usalama iko imara na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha amani inatawala wakati wote wa uchaguzi.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Mufindi Kusini, David Kihenzile, amesema endapo ataendelea kupata ridhaa ya wananchi kwa muhula mwingine, atapigania utekelezaji wa miradi ya barabara ili kuboresha miundombinu ndani ya jimbo hilo.

 “Barabara za vijijini na zile zinazounganisha maeneo ya kiuchumi hazipaswi kubaki kikwazo. Kuna barabara ziko kwenye usanifu na mkandarasi anasubiri malipo ili kuanza kazi. Hatutaacha agenda ya barabara,” alisema.

Amesema katika sekta ya nishati, mafanikio makubwa yamepatikana ambapo mwaka 2020 vitongoji vyenye umeme vilikuwa chini ya 100 kati ya 325, lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 75 ya vitongoji hivyo vimeunganishiwa umeme na kubakiwa na 86 pekee.


Katika afya, Kihenzile alibainisha kuwa vituo vya afya vimeongezeka na vingine vipo katika hatua za mwisho kukamilika, huku akiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa huduma za kijamii ikiwemo michezo, ajira na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia ruzuku ya mbolea

Naye Mbunge Mteule wa Baraza la Vijana (UVCCM), Jasmini Ng’umbi, amewahimiza wananchi wa Mufindi Kusini kujitokeza mapema Oktoba 29 na kukipa heshima Chama Cha Mapinduzi kwa kura za ndiyo.

 “Twende tukamchague Dkt. Samia, tumchague Kihenzile na madiwani wote wa CCM. Mmeona maendeleo yaliyofanyika, hivyo tuendelee kuyaimarisha kwa kumchagua anayeyajua mahitaji yenu,” alisema.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI