Header Ads Widget

RAIS MWINYI :SMZ IMEDHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI WOTE


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma bora za afya katika kila ngazi ya utoaji huduma nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Oktoba 2025, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la huduma za akina mama na watoto katika Hospitali ya Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za Wilaya na Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Saratani ya Binguni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bora, za uhakika na zinazopatikana kwa wakati.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho cha Makunduchi kutaleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya katika Mkoa wa Kusini, hususan kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga, kwa kuwa kutapunguza changamoto zilizokuwepo awali wakati wa kujifungua.

Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru wafadhili wa mradi huo wakiwemo Taasisi ya Fumba Port, Lady Fatuma Foundation, na Jaffer Foundation, kwa mchango wao mkubwa wa kifedha na moyo wa kujitolea kusaidia Serikali katika uboreshaji wa huduma za afya.

Amesema Serikali inatambua kuwa haiwezi kutekeleza kila jambo peke yake, hivyo ushirikiano kutoka kwa wadau wa maendeleo na taasisi binafsi ni muhimu katika kuinua ustawi wa jamii, hasa katika kuokoa maisha ya akina mama na watoto.


Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi  amemuagiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa kuzingatia viwango vya ubora na kwa muda mfupi zaidi, akisisitiza kuwa muda wa ujenzi unapunguzwe kutoka mwaka mmoja hadi miezi tisa kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Mngereza Miraji Mzee, amesema ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na Kampuni ya Quality Building Constructor kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5, na ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto.

Vilevile, amesema takriban wananchi 9,821 kutoka shehia 21 za Wilaya ya Kusini watanufaika na huduma zitakazotolewa katika kituo hicho, zikiwemo huduma za uzazi salama, huduma za ultrasound, huduma za watoto wachanga, na huduma za maabara.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI