Header Ads Widget

DC SUMAYE AONGOZA MAOMBI YA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU


Na Ashrack Miraji Matukio Daima 

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye, ameongoza kongamano maalum la amani lililofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, likiwa na lengo kuu la kuliombea Taifa na Wilaya ya Lushoto kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Akizungumza mbele ya viongozi wa dini, serikali, na wananchi, Mhe. Sumaye alisema amani ni msingi wa ustawi wa taifa lolote na inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote.

Mhe. Sumaye alisema serikali ya Wilaya ya Lushoto imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na usalama, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuwa balozi wa amani. Aliongeza kuwa kipindi cha uchaguzi si muda wa kugombana bali wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa heshima na upendo.

Akiendelea kueleza, Mhe. Sumaye alisisitiza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuepuka lugha za chuki na misimamo inayoweza kugawa jamii. “Tujenge hoja za kimaendeleo, si maneno yanayovunja undugu wetu. Amani ya nchi hii ni urithi tuliopokea kutoka kwa waasisi wa Taifa, tusiiweke rehani kwa siasa za muda mfupi,” alisema.


Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuiombea nchi na kuwaelimisha waumini juu ya umuhimu wa kudumisha amani wakati wote wa kampeni na upigaji kura. Alisema maombi ni silaha muhimu inayoweza kuunganisha wananchi bila kujali tofauti za kiimani au kisiasa.

Mhe. Sumaye pia aliwahimiza vijana kutumia nguvu zao katika kuleta maendeleo badala ya kutumika kuvuruga amani. “Vijana wetu ni nguzo ya taifa. Mnapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si chanzo cha migogoro. Tuitumie mitandao ya kijamii kuhubiri amani na kuelimisha jamii, si kueneza chuki,” aliongeza.


Aidha, alitoa rai kwa wananchi wote wa Lushoto kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha mazingira yanabaki tulivu kabla, wakati, na baada ya uchaguzi. Alisema ushirikiano huo utawezesha Wilaya ya Lushoto kuendelea kuwa mfano wa amani na utulivu nchini.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Sumaye aliwashukuru viongozi wote wa dini na serikali walioshiriki katika kongamano hilo, akiwataka kuendeleza maombi na mazungumzo ya kudumisha amani. Baada ya hotuba, aliongoza sala maalum ya kuliombea Taifa.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI