Na Moses Ng’wat, Songwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amesema Jeshi hilo limeimarisha ulinzi kwa raia na mali zao kabla, wakati na baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, huku likieleza kuwa limeendelea kufanya ufuatiliaji wa mienendo ya matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii (cyber patrols).
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 27, 2025, Kamanda Senga alisema hadi sasa hakuna dalili zozote za uvunjifu wa amani katika mkoa huo, na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuwajibika kikamilifu kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi kwa amani na utulivu, hivyo tunawahimiza wananchi wote kujitokeza kupiga kura kwa utulivu, kwani huu ni wajibu wa kikatiba,” alisema.
Aidha, Kamanda Senga alibainisha kuwa mikakati thabiti ya kiulinzi kwa kushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, Tume ya Uchaguzi, viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi za kiraia na wadau wa amani ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limeimarisha doria katika vituo vyote vya kupigia kura, barabara kuu na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, sambamba na kufanya (Cyber Patrols) kufuatilia mienendo ya matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii.
"Tumeanza kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaotumia mitandao kueneza chuki na migawanyiko katika jamii, tunawasihi Wananchi watumie mitandao kujenga amani, uzalendo na mshikamano,” alisema Kamanda Senga.
Vile vile aliwataka wananchi, wanasiasa, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wadau wote wa demokrasia kuendelea kushirikiana kwa amani na kufuata sheria za nchi katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Hata hivyo, Jeshi hilo limekumbusha kuwa suala la kudumisha amani ni jukumu la kila mmoja, na kwamba limeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii katika kulinda utulivu wa Mkoa wa Songwe.
Pia limetoa onyo kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uchochezi, uvunjifu wa amani na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
"Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya vitendo hivyo vya ukiukwaji wa sheria, hivyo niwaombe wananchi wote katika mkoa wetu kutii sheria za nchi bila shuruti" alisisitiza Kamanda Senga.





0 Comments