Header Ads Widget

CWT YAWAHAKIKISHIA WATANZANIA USHIRIKI WA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025

 

Chama cha waalimu nchini Tanzania CWT kimewataka waalimu kote nchini kuendelea na msimamo wao wa kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba, 2025 kwenda kupiga kura kwani ndiyo msimamo wa Chama ambao ulikwisha tolewa na Msemaji wa Chama hicho ambaye ni Rais wa Chama Cha waalimu nchini Tanzania Bw. Suleiman Ikomba.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CWT Mwalimu Joseph Misalaba kwenda kwa Makatibu wa CWT, Mikoa na Wilaya imesisitiza waalimu pia na umma kwa ujumla kuwa Mabalozi wazuri wa Upendo, amani, umoja na mshikamano kwaajili ya maendeleo thabiti ya Tanzania kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye, wakiishukuru pia serikali kwa kuendelea kutatua kero za waalimu kwa kushirikiana na CWT.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa CWT imekuja baada ya kuzuka kwa uvumi mitandaoni zikieleza kuwa Chama Cha Waalimu kimesusia uchaguzi Mkuu wa Keshokutwa Jumatano, ambapo Mwalimu Misalaba amekanusha taarifa hizo na akitaka Watanzania wazipuuzie.

"Chama Cha Waalimu Tanzania kinapenda kukanusha kwa nguvu zote taarifa zinazosambaa kupitia Mitandao ya kijamii na kwenye baadhi ya Vyombo vya habari ikihamasisha walimu kutoshiriki kwenye shughuli za uchaguzi Mkuu ambazo baadhi ya waalimu hutumika kama wasaidizi wa shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za serikali ya Tanzania." Amesema Katibu Mkuu huyo.


Mwalimu Misalaba pia ametoa rai kwa waalimu, wamachama wa CWT na watanzania wote kwa ujumla kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wala msingi wowote, akisema zinalenga kuleta taharuki, uzushi na uchonganishi ambao unapaswa kupingwa kwa nguvu zote ili kuendelea kulinda amani, umoja na utulivu ambao ni tunu ya Taifa.

CWT imewahakikishia waalimu, serikali na wananchi wote kuwa kitaendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha kuwa tabia ya utoaji wa taarifa potofu inakomeshwa ili kulinda misingi na madhumuni ya uwepo wa vyama vya Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI