.jpg)
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Kundo Andrea Mathew, amewataka wananchi kuchagua viongozi wanaotokana na CCM ili waendelee kuwaletea Maendeleo.
Akizungumza kwenye Mkutano ya kampeni iliyofanyika Mitaa ya Bunamhala (Kata ya Bunamhala) na Wala (Kata ya Isanga), amesema kuwa serikali bapo ameeleza mafanikio yaliyofikiwa na kutoa ahadi mpya za maendeleo.
Mhandisi Kundo ameahidi endapo atachaguliwa atahakikisha Ujenzi wa Daraja la Mto Ndoba (Bunamhala) na Daraja la Mto Ng'watungu (Isanga) unakamilika ili kuboresha mawasiliano na kufungua fursa za kiuchumi.
Amesema atahakikisha wanaimarisha huduma za maji safi, kwa kupanua mtandao wa mabomba na kuongeza pampu mpya karibu na makazi ya wananchi.
"Tutasimamia Mradi wa umeme wa kupeleka nguzo hadi kwenye makazi ya watu, ili kuhakikisha kila kaya inapata nishati hiyo muhimu" amesema Mhandisi Kundo.
Aidha, alieleza kuwa Kata ya Bunamhala imekuwa kinara wa kupata fedha nyingi za miradi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya na barabara za mitaa.
Eng. Kundo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kwenda kupiga kura na kuchagua CCM kwa nafasi zote, huku akisisitiza kuwa maendeleo ya Bariadi Mjini yamejengwa juu ya misingi ya uongozi wa CCM.
Mhandisi Kundo amewakaribisha wananchi wote wa Bariadi Mjini kushiriki mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yatakayofanyika tarehe 10 Oktoba 2025 katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Amewataka wakazi wa maeneo yote kujitokeza kwa wingi kuonyesha mshikamano na kumuunga mkono Rais katika juhudi za kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Mwisho.
0 Comments