Na Mwandishi wetu.... Matukio daima
KAMANDA wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga amesema jeshi lake limejipanga ipasavyo kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
Amesema kuwa hakuna maandamano yoyote yatakayofanyika siku ya uchaguzi kama inavyoenezwa na baadhi ya watu hususani mitandaoni.
Kamanda Benjamin Kuzaga ameeleza hayo wakati akizungumza na watumishi, wananchi na wanafunzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya katika mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya.
Amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye matembezi ya kusherehekea ushindi wa tuzo ya mwenge kikanda katika Halmashauri ya Mbeya na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ameeleza kuwa kumekuwepo na baadhi ya maneno katika mitandao ya kijamii kuwa Oktoba 29 kutakuwa na maandamano lakini hayana kibali chochote hivyo kabla ya kudai haki lazima mtu au watu watimize wajibu hivyo kuwasisitiza wananchi kuwa hakutakuwa maandamano yoyote bila kibali katika Halmashauri ya wilaya ya Mbeya na mkoa wa Mbeya kwa ujumla.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Erica Yegella, amewashukuru watumishi na wananchi katika Halmashauri ya Mbeya kwa ushirikiano katika kujenga na kutunza miradi wilayani Mbeya hata kupata tuzo hiyo na kuwaasa kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu na kurudi majumbani mwao siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Mwisho.










0 Comments