Header Ads Widget

KAMISHNA KUJI ASHIRIKI KIKAO KAZI CHA MWAKA CHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA UHIFADHI NA UTANGAZAJI WA VITUO VYA MALIKALE


Na Philipo Hassan - Dodoma.

Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, Oktoba 25, 2025, ameshiriki katika kikao kazi cha Kitengo cha Malikale zilizokasimiwa kwa TANAPA kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kilijadili utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na tathmini ya robo mwaka ya kwanza kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Kuji aliwapongeza wasimamizi wa vituo vya malikale vinavyosimamiwa na TANAPA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza uhifadhi wa urithi wa kihistoria na utamaduni wa Taifa.

“Endeleeni kubuni vyanzo vya mapato yatokanayo na  shughuli za utalii zinazofanyika katika maeneo yetu ya malikale, imarisheni usimamizi, utendaji kazi pamoja na uwajibikaji katika majukumu kwa kuhakikisha mnafuatilia na kuboresha miundombinu iliyopo katika vituo ili kuifanya idumu kwa muda mrefu na kuendelea kuhifadhi malikale hizi kwa faida ya kizazi hiki na kizazi kijacho” alieleza Kamishna Kuji.



Awali, Afisa Uhifadhi Mkuu na Mratibu wa Malikale zilizokasimiwa TANAPA, Neema Mbwana alimkaribisha Kamishna Kuji na kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kitengo hicho. Pia Mbwana alieleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 na robo ya kwanza ya 2025/2026, kumekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za uhifadhi, utafiti na utalii wa urithi asilia katika vituo vya malikale zilizokasimiwa kwa TANAPA.

Mbwana alibainisha kuwa kumekuwa na maendeleo katika vituo vya malikale, ikiwemo kuimarika kwa miundombinu ya vituo kama ukarabati wa majengo, kuongezeka kwa idadi ya wageni na mapato. “Kwa kipindi hicho, jumla ya wageni 31,054 walitembelea vituo vyetu na kuingiza zaidi ya shilingi milioni 79.8,” Mbwana aliongeza.

Mafanikio mengine yaliyoelezwa ni pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa urithi wa utamaduni wa malikale na kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa. “TANAPA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa kama UNESCO, ICOM, ICCROM na ICOMOS katika miradi ya urithi wa dunia ambapo kupitia ushirikiano huo Njia ya Kati ya Utumwa (Central Slave Trade Route) imeingizwa kwenye orodha ya UNESCO (Tentative List) ambapo Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika (AWHF) umetoa ufadhili kwa ajili ya maandalizi ya mkakati wa kutangaza  njia hiyo rasmi kama Urithi wa Dunia.” Alieleza Bi Mbwana.



Aidha, kituo cha zama za mawe za kale cha Isimila  kilipata ushindi wa kimataifa kupitia wasilisho la “Bridging Continents to Safeguard Deep Time” nchini Italia hatua iliyotangaza TANAPA kimataifa kama taasisi inayoendeleza tafiti za kiakiolojia kwa viwango vya juu.

Kikao hicho kilihusisha mawasilisho ya  wakuu wa vituo vya Malikale ambavyo ni kituo cha Zama za Mawe Isimila (Iringa), Makumbusho la Chifu Mkwawa (Kalenga), Nyumba Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere (Dar es Salaam), Makumbusho la Biashara ya Watumwa Caravan Serai (Bagamoyo), pamoja na Makumbusho la Dkt. Livingstone (Ujiji, Kigoma).

Vituo vya malikale vilivyokasimiwa kwa TANAPA vimeendelea kupata mafanikio mbalimbali ambapo idadi ya watalii wanaotembelea vituo hivyo pamoja na mapato yameendelea kuongezeka. Pia, miundombinu ya vituo hivyo imeendelea kuimarika na Shirika linaendelea kuweka jitihada za kuboresha vituo hivyo. 

Vituo vya malikale ni chachu ya maendeleo na vinaendelea kutumika katika kutoa elimu ya uhifadhi wa malikale na historia ya nchi  kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi ambapo elimu hiyo inatoa chachu kwa kundi la vijana kuweza kufahamu zaidi historia ya nchi ya Tanzania.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI