Marehemu Bi Elizabeth Michael Mushi (MAZERI)enzi za uhai wake
Matukio Daima, Moshi
Kutoka kwenye machozi ya majonzi, sasa kunachipua matumaini mapya kwa jamii. Hicho ndicho kinachoendelea kijiji cha Kitandu, Kata ya Uru Kusini wilayani Moshi,mkoani Kilimanjaro baada ya familia ya marehemu Elizabeth Michael Mushi kuamua kugeuza kumbukumbu ya mama yao kuwa zawadi kwa jamii kwa kuanzisha taasisi ya kijamii ijulikanayo kama Elizabeth Foundation.
Taasisi hiyo inayoanzishwa mara baada ya kuvunjwa Tanga la marehemu, inalenga kutoa huduma za elimu, uchunguzi wa afya, vipimo na matibabu bure kila mwaka ifikapo Oktoba 3, siku ambayo marehemu alifariki dunia, ikiwa ni njia ya kudumisha alama ya upendo na kujitolea aliyoyaishi enzi za uhai wake.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Mhandisi Stratton Anizety,akizungumza kwenye Ibada ya kuvunja Tanga la Marehemu Mama yao, alisema wazo hilo limetokana na historia ndefu ya mateso aliyoyapitia mama yao kutokana na maradhi kwa zaidi ya miaka 11, lakini bado hakuwahi kupoteza moyo wa huruma kwa wengine.
> “Mama alituonyesha kuwa maumivu si sababu ya kuacha kutenda mema. Tulipoona alivyoteseka lakini bado aliendelea kuwajali wengine,aliwasomesha watoto zaidi ya 10 wasio na uwezo, tulijua tunapaswa kuendeleza urithi huo,” alisema Mhandisi Stratton
Alibainisha kuwa huduma hizo zitaanza kutolewa katika vijiji vya Kata ya Uru Kusini kabla ya kupanuka zaidi mkoani Kilimanjaro, zikilenga kutoa vipimo na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza hasa shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Gaudens Mushi, mtoto mwingine wa marehemu, alisema tatizo kubwa nchini ni watu kutochukua tahadhari mapema kuhusu afya zao.
> “Wengi wetu tunasubiri tuugue ndipo tukimbie hospitali. Hii taasisi itatusaidia kujenga tabia mpya ya kujua afya zetu mapema kabla maradhi hayajawa makubwa,” alisema.
Naye Mwalimu Gundelinda Anizety, alisema mpango huo unalenga kuwafikia watu wasio na uwezo wa kupata huduma za afya kutokana na umbali au gharama.
> “Kuna watu vijijini hawajawahi kufika hospitali kwa muda mrefu kwa sababu hawana nauli wala bima. Tunataka kuwaletea huduma hizo hadi walipo,” alisisitiza
Kwa upande wake, Bi. Alice Cyprian Mndeme, mkwe wa marehemu, alisema Elizabeth Foundation imejengwa juu ya nguzo sita alizoishi nazo marehemu.
> “Mama Elizabeth alipenda sala, alihubiri upendo, alisisitiza elimu, afya, maendeleo na ndoa zenye amani. Tumebeba urithi huo kuwa dira ya taasisi,” alisema Bi. Alice kwa hisia.
Akitoa elimu ya afya kwa waombolezaji, Dkt. Timon Emaely, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya KCMC, alionya juu ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
> “Tunapaswa kuwafikia wananchi vijijini ili wengi wajitambue na kuchukua hatua mapema kabla ugonjwa haujazidi na kushindwa kutibika, Afya ni wajibu wa kila mmoja, si mpaka uwe na dalili ndipo ujue unaumwa, lakini tufanye mazoezi ya mara kwa mara kuweka miili yetu vizuri,” alisema Dkt. Timon.
Nao viongozi wa eneo hilo wamesema familia hiyo imeandika historia. Wakili Wilhard Kitali, Diwani mstaafu wa Uru Kusini, alisema yupo tayari kusaidia upande wa kisheria kuhakikisha taasisi inasajiliwa haraka.
> “Familia hii imeweka mfano wa nadra.hata Mimi ni miongoni mwa wanufaika, kwamaana hiyo Nitahakikisha ndani ya siku saba tunapata usajili rasmi wa Elizabeth Foundation ili wengi wanufaike,” alisema Wakili Kitali.
Wananchi wa eneo hilo pia wamepongeza hatua hiyo wakisema imewapa tumaini jipya.
Valeria Petter Mringo alisema:
> “Kwa mara ya kwanza tunaona huduma kama hizi zikianzishwa na familia binafsi. Hii ni faraja kubwa kwa jamii ya Uru.”
Anneth Munuo naye alisema:
> “Kila mtu atapaswa kuchukua jukumu la kupima afya yake. Tukijua mapema, tutapunguza vifo vya presha na kisukari.”
Vitalis Karia aliongeza:
> “Hii siyo tu taasisi ya kumbukumbu, ni mwamko wa afya. Tunashukuru familia ya marehemu kwa moyo huu wa kipekee.”
Wananchi hao walisema kuanzishwa kwa Elizabeth Foundation kutasaidia kujenga utamaduni wa kupima afya kwa hiyari, kupata elimu sahihi ya afya, na kuchukua hatua kabla ya maradhi kuathiri maisha.
0 Comments