Na Samwel Mpogole MBEYA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekabidhi mashine mbili muhimu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaozaliwa chini ya uzito na kabla ya kufikia muda wao wa kuzaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
Mashine hizo zimekabidhiwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila, ambaye ameeleza kuwa msaada huo umetolewa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dkt. Godlove F. Mbwanji, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akieleza kuwa vifaa hivyo vitaboresha kwa kiwango kikubwa huduma kwa watoto njiti na wenye changamoto za kiafya mara baada ya kuzaliwa.
Naye Mkuu wa Idara ya Watoto katika hospitali hiyo, Dkt. Nazareth Mbilinyi, amesema kuwa zaidi ya nusu ya watoto wanaozaliwa hospitalini hapo huzaliwa wakiwa na uzito pungufu au kabla ya muda wao, huku wengine wakikumbwa na changamoto ya ugonjwa wa manjano. Ameongeza kuwa ujio wa mashine hizo ni faraja kubwa kwa timu ya madaktari na wauguzi wanaohudumia watoto hao kwani sasa watakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora zaidi kwa wakati muafaka.
Baadhi ya wazazi waliokuwa wakihudumiwa katika kitengo hicho wameeleza kufurahishwa na msaada huo, wakisema kuwa utaokoa maisha ya watoto wengi na kupunguza hofu wanayoipata pindi watoto wao wanapozaliwa wakiwa na hali tete.
Mashine hizo zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma katika wodi ya watoto wachanga, na hivyo kuunga mkono jitihada za serikali katika kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini.
0 Comments