MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema serikali imepanga kujenga bandari ya uvuvi ya kisasa katika eneo la Kihinani na kuongeza viwanda vitakavyowezesha kuongeza thamani ya mazao samaki, dagaa na mazao mengine ya baharini.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza na wajasiriamali, wakulima, bodaboda na wavuvi wa Mkoa w Magharibi "A" wanaotoka katika uwanja wa mpira Chuini ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake.
Alisema viwanda hivyo vitajengwa katika eneo la Fungurefu ili kuongeza thamani ya mazao na wavuvi waweze kupata tija ya mazao wanayozalisha na kupata soko la uhakika.
Alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuimarisha sekta ya uvuvi, kuinua maisha ya wavuvi wadogo na kuongeza thamani ya mazao ya baharini.
Aidha alisema kiwanda hicho kitatoa ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa bidhaa za wavuvi wa Zanzibar.
"Tunataka kuona wavuvi wetu hawapotezi ten mazao yao kwa kukosa soko au vifaa vya kuhifadhi kwani kupitia kiwanda hicho samaki na dagaa watasindikwa kisasa na kuuzwa ndani na nje ya nchi," alisema.
Mgombea huyo alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kukuza uchumi wa buluu na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara ya bidhaa za baharini.
Aliahidi kuwa serikali itaendeleza ujenzi wa masoko ya samaki, madiko na kuongeza viwanda vya kuuongeza thamani ya dagaa na itaongeza kutoa vifaa vya uvuvi ikiwemo boti na zana nyengine za uvuvi
Hata hivyo, alisema serikali imeweka mazingira mazuri ya masoko ikiwemo Chuini, Jumbi, Mwanakwerekwe na Mombasa linaendelea huku itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wajasiriamali kwani wengi ambao wanahitaji maeneo hayo kwani masoko yaliyojengwa bado hayajakidhi haja.
"Tutaendelea kujenga masoko wilayani mikoani na haya makubwa kuona kila mjasiriamali na mfanyabiashara anafanya biashara zake katika mazingira mazuri na kutoa mafunzo kwa taasisi zinazotoa mikopo ili kuwawezesha watu kufanya biashara zao vizuri, mafunzo ya alama za ubora yanatayowawezesha bidhaa zao kuwa na thamani zaidi," alisema.
Alisema serikali pia itaongeza fungu la mikopo isiyokuwa na riba ili wale wote ambao hawajafikiwa waweze kufikiwa kwa asilimia kubwa.
Akizungjmzia tozo wanazotozwa wafanyabiashara katika masoko Dk.Mwinyi alisema lengo ni kujenga masoko kuwarahisishia biashara zao hivyo atahakikisha analisimamia ili tozo hizo ziwe rafiki zaidi.
0 Comments