Header Ads Widget

POLISI MWANZA YAWATAKA WANANCHI KUPIGA KURA NA KUREJEA NYUMBANI.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura oktoba 29 Mwaka huu na kisha kurejea nyumbani mara baada ya kumaliza zoezi la upigaji kura.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 27, kamanda wa Jeshi hilo Wilbroad Mtafungwa, ameeleza kuwa ni umuhimu Kila mwananchi  kufuata utaratibu wa kwenye vituo vya kupigia kura ili kuepuka makundi yanayoweza kuleta uvunjifu wa amani.

 "Wananchi wanapaswa kupiga kura na kisha kurudi nyumbani, na wasibaki katika vituo vya kupigia kura hii itasaidia kuepuka hali yoyote ya usumbufu au machafuko," alisema Kamanda Mtafungwa.

Mtafungwa ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu, na kusisitiza kuwa Jeshi hilo litafanya doria za miguu na magari  katika maeneo yote ya uchaguzi ili kudhibiti vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.

 "Jeshi la Polisi lipo kwenye maeneo yote ya kupigia kura, na tunafanya doria katika maeneo ya mijini na vijijini tunahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa amani," alisema  Mtafungwa.

Aidha ameeleza kuwa hawataruhusu makundi yoyote kuendelea kukaa kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kumaliza kupiga kura, kwani hali hiyo inaweza kuchochea machafuko na uvunjifu wa amani. 

"Tunawaomba wananchi waache kutumia vituo vya kupigia kura kama maeneo ya kujikusanyia. Baada ya kupiga kura, ni muhimu waondoke na warejee nyumbani," alisisitiza.

Kamanda Mtafungwa aliongeza kuwa hali ya usalama katika Mkoa wa Mwanza ni shwari, na Jeshi la Polisi limeajizatiti kuhakikisha kuwa uhalifu wa aina yoyote haujitokezi

 "Tunajivunia ushirikiano wa wananchi wetu katika kuzuia uhalifu, na tutaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu watakaohatarisha amani," alisema Mtafungwa.

Aidha amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza na wageni kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu uhalifu ili kuendelea kudumisha amani hadi baada ya uchaguzi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI