Na, Jusline Marco:Arusha
Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2024 ya Shirika la Utalii Duniani kuhusu mwenendo wa utalii duniani limeitaja nchi ya Tanzania kuwa moja ya nchi zilizoongoza Afrika kwa mwaka 2024 kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii kwa asilimia 48, ikifuatiwa na Ethiopia asilimia 40,Morocco asilimia 35,Kenya asilimia 11 na Tunusia asilimia 9 ambapo pia katika ripoti ya mwaka 2025 Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 20 Bora Duniani zinazofanya vizuri katika utalii kwa wastani wa zaidi ya asilimia 50.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas ameyasema hayo Sept 27 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani iliyofanyika katika Kreta ya Ngorongoro ambapo amesema kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Julai 2025 idadi ya watalii imeendelea kuongezeka na kufikia milioni 1.27 sawa na asilimia 9.2 ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2024 ambapo watalii walikuwa milioni 2.5.
Dkt. Abbas amesema wizara ya utalii itaendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya uendelezaji wa utangazaji utalii ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ikiwa ni pamoja na kutumia fursa za ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo huduma za usafirishaji,fursa za Tehama na huduma ya biashara ambapo serikali itaendelea kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua, kuwa shindani na yenye kujumuisha jamii katika ukuaji wake.
Aidha amesema hali ya sekta ya utalii nchini imekuwa ikihamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za utalii kwa kuzingatia sera ya taifa ya utalii ya mwaka 1999, sheria ya utalii namba 65, mikakati na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha wananufaika na ukuaji wa sekta ya utalii ambapo amewataka wadau wa utalii wa umma na binafsi kuendelea kushirikiana na wizara katika uendelezaji na utangazaji utalii.
Ameongeza kuwa hali ya utalii nchini imeendelea kukua na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi ambapo idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 kwa mwaka 2021 hadi kufikia watalii milioni 2,141,895 kwa mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 132.1 huku idadi ya watalii wa ndani ikiwa ni 3,218,352 kwa mwaka 2024 kutoka watalii 788,933 kwa mwaka 2021 na kufanya kufikia jumla ya idadi ya watalii wa ndani na nje milioni 5,360,247 kwa mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 107.2.
Vilevile amesema mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kwa asilimia 200 mwaka 2024 kutoka dola za kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 3.9 mwaka 2024 ambapo amesema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji madhubuti wa malengo ya ilani ya uchaguzi ya ccm ya mwaka 2020/25 kuhusu kufikia idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
Sambamba na hayo amesema katika mnyororo wa thamani, utalii umeendelea kuimarika ukihusisha shughuli za uwekezaji katika biashara za huduma za utalii na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na kuendelea kutoa fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja takribani milioni 1.6 .
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na jitihada mbalimnali za uendelezaji wa mazao ya utalii, uboreshaji wa miundombinu, matumizi yakinifu ya Tehama katika utalii ,shughuli za utangazaji utalii ndani na nje ya nchi, chini ya serikali ya awamu ya sita ikijumuisha filamu ya Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania ambapo nchi ya Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa na kuweza kupata tuzo za utalii za World Travel Awards zinazotolewa na World Luxury Media Group Limited.
Katika hatua nyingine Dkt. Abbas amesema utoaji wa Tuzo za Uhifadhi na Utalii zinazojulikana kama The Serengeti Awards , itakayofanyika Desemba 19 mwaka huu jijini Arusha zimelenga kutambua, kuheshimu na kusheherekea mchango wa wadau mbalimbali wa sekta ya Uhifadhi na Utalii Tanzania ambapo tuzo hizo zilizinduliwa mwaka jana Desemba 20 na tuzo za heshima kutolewa kwa baadhi ya wadau katika utambulisho wake.
Amebainisha kuwa jumla ya tuzo 56 zilizo katika makundi 7 zitatolewa ambapo dirisha la upokeaji wa maombi ya ushiriki wa kuwania tuzo hizo litafunguliwa Oktoba 10 hadi 31 mwaka huu kupitia tovuti rasmi ya wizara na wadau wenye sifa wataweza kushiriki huku mchakato wa utoaji wa tuzo hizo utahakikisha uwazi, usawa na ushindani wa haki.
Mwisho.









0 Comments