Na Mwandishi Wetu, Matukio Daima App Chalinze
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze Wilaya ya Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete ameahidi kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha huduma ya upatikanaji maji itapatikana kwa asilimia 100.
Ridhiwani alitoa ahadi hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ubunge Jimbo la Chalinze kwenye uwanja wa Mdaula.
Alisema kuwa huduma hiyo ya maji itazifikia kaya zaidi ya 300,000 kutoka kaya zaidi ya 90,000 kwa miaka mitano iliyopita ambapo maji yanapatikana kwa asilimia 92.
"Nikichaguliwa nitakabiliana na moja ya changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kuwafikishia wananchi majumbani badala ya vioski na kuzifikia kaya hizo 300,000,"alisema Kikwete.
Alisema kuwa atahakikisha kunaletwa miradi ya maji ambayo itapeleka maji majumbani badala ya matumizi ya vituo vya maji kuwa na mradi wa uwekaji wa taa za barabarani.
"Kwa upande wa miundombinu tutanunua greda kwa ajili ya kuchonga barabara na kujenga vituo vinne vya mabasi, ujenzi wa hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota nne ambayo itakuwa na ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuongeza mapato,"alisema Kikwete.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani Zainabu Vullu alisema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ni Mwanadiplomasia mahiri duniani na ameahidi akichaguliwa kupitia ilani ya 2025-2030 atahakikisha anaboresha huduma za afya, elimu, miundombinu.
Kwa upande wake Mratibu wa kampeni kanda ya Pwani Richard Kasesela alisema kuwa watu waliojiandikisha wahakikishe wanajitokeza kuwapigia kuwa wagombea wa CCM.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo Abubakar Mlawa alisema kuwa chama kimejipanga kuhakikisha Rais anapata kura za kishindo sambamba na Wabunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete na Bagamoyo Subira Mgalu na Madiwani wa Kata 15 za Chalinze.
0 Comments