Header Ads Widget

NCAA YATAKIWA KUFUATA SHERIA,TARATIBU NA KANUNI KATIKA UWAJIBIKAJI WAO.

 


Na Jusline Marco, Arusha


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi ameitaka menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha kuendelea kusimamia uwajibikaji kwa kufuata sheria,taratibu na kanuni.


Dkt. Abbasi ametoa rai hiyo katika kikao chake na menejimenti ya mamlaka hiyo mara baada ya ukaguzi wa mradi wa Makumbusho ya Jiolojia na jengo la ofisi ya Makao Makuu ya Ngorongoro ambapo amesema jukumu la kila mtumishi wa umma liwe ni kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuleta tija kwa taifa.


“Simamieni watumishi walio chini yenu katika kusimamia uhifadhi,utalii na maendeleo ya jamii ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo”,alisema Dkt. Abbasi.


Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo anayeshughulikia uhifadhi,utalii na maendeleo ya jamii Joas Makwati katika taarifa yake alisema kuwa mamlaka imejipanga kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo kukuza uhifadhi,utalii na maendeleo ya wananchi.


Katika hatua nyingine Dkt. Abbasi wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu elimu ya utalii wa anga  yaliyoanza Septemba 19 mwaka huu Wilayani Karatu Mkoani Arusha, Mafunzo yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, amesema utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Maliasili na utalii kufungua mazao mapya utalii ikiwepo utalii wa Anga ambapo hatua ya sasa ni kutoa mafunzo, maarifa na ujuzi kwa watanzania kuhusu utalii wa anga, vifaa vinavyotumika na fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii. 


Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania Prof. Saganga Kapaya ameeleza kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za utalii wa anga, ambao ni bidhaa mpya ya utalii hapa nchini kwa kuwa zaidi ya theluthi moja ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa, na hivyo kupelekea maeneo yake mengi kuwa na anga lenye giza wakati wa usiku hivyo kuwezesha anga kuonekana kwa zaidi ya asilimia 95 ukilinganisha na mataifa mengine Afrika. 


Naye Prof. John Hearnshaw kutoka New Zeland ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo ameeleza kuwa mafunzo yatajikita katika maeneo manne ambayo ni namna ya kuendesha utalii wa anga kwa kushirikisha wadau wa utalii na Jamii, utalii wa anga na Fizikia anga, matumizi ya Telescopic pamoja na upigaji wa picha za utalii wa anga.


Mafunzo hayo yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 70, ambao ni wasafirishaji watalii, waongoza watalii, waendeshaji wa huduma za malazi, taasisi za serikali zinazohusika na kutangaza utalii (TTB na ZCT), taasisi za uhifadhi (NCAA, TANAPA, TAWA, na TFS), taasisi za elimu, mafunzo na utafiti (NCT, ACWM-Mweka, VETA, na OUT), Wataalamu wa Utalii, Wasimamizi wa Utalii, Watafiti, Waandaaji wa sera na wafanya maamuzi, Wana-astronomia, Wanafunzi, Wajasiriamali, na watunga sera.


Mwisho.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI