Header Ads Widget

LISSU ASOMEWA SHITAKA LA UHAINI KWA MARA YA KWANZA, KESI YAHAIRISHWA HADI OKTOBA 6

 

Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam imesoma shitaka linalomkabili Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini. Lissu amesomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza Mahakama kuu mbele ya jopo la majaji na kukana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 6, 2025, baada ya upande wa utetezi kutoa orodha ya mashahidi wake. Awali, Mahakama ilikuwa imetupilia mbali hoja zote za pingamizi la Lissu kuhusiana na uhalali wa hati ya mashtaka.

Lissu alihoji kuwa hati ya mashtaka haionyeshi maelezo ya kosa wala nia ya kutenda uhaini, vipengele ambavyo ni muhimu katika kesi ya aina hiyo.

Hata hivyo, Jaji Dunstan Ndunguru alieleza kuwa Mahakama imeridhika hati ya mashtaka ipo sahihi na inatoa maelezo ya kosa kama sheria inavyotaka. Suala la nia ya kutenda kosa hilo litaamuliwa kupitia ushahidi unaotarajiwa kuwasilishwa mahakamani.

Kuhusu pingamizi la Lissu kuhusu maelezo ya mashahidi na utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya kuwalinda mashahidi wa Jamhuri, Mahakama ilibainisha kuwa hoja hizo zinahusu mwenendo wa awali wa kesi (committal proceedings) na tayari zimepatiwa uamuzi.

Hivyo, pingamizi la Lissu halina msingi na kesi ya uhaini itaendelea Oktoba 6, 2025. Katika hatua nyingine Mahakama hiyo pia imekataa ombi la Lissu la kutaka kesi hiyo irushwe mubashara, kwa kusema hakuna kanuni zinazozimamia usikilizwaji wa kesi mubashara.

Septemba 15 Mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi la Lissu, kuhusu Mamlaka ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi yake ya uhaini, Mahakama ikisema ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo

"Mahakama baada ya kupitia hoja za pande zote imeridhika kuwa mapingamizi haya hayawezi kuharibu mwenendo mzima wa Mahakama ya Ukabidhi na kuifanya Mahakama hii kukosa mamlaka. Hivyo sababu hii ya pingamizi inakataliwa," amesema Jaji Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) wakati akisoma uamuzi huo baada ya kujadili hoja zote.

Katika pingamizi lake Lissu alidai kuwa Mahakama hiyo (Mahakama Kuu) haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo huku akibua hoja tano kuu:

Mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi.

Mashitaka yanayomkabili Lissu ni ya kisiasa na hayana msingi wa kisheria.

Hukumu ya awali na machakato wake wote katika Mahakama ya ukabidhi (Kisutu) haipaswi kuendelea kuwa na nguvu ya kisheria.

Ana haki ya msingi ya kikatiba ya usikilizaji wa haki bila masharti.

Anaomba kesi ifutwe mara moja na kuachiliwa huru bila masharti yoyote

Tundu Lissu alikamatwa Aprili 9, 2024, Mimba na kupelekwa Dar es Salaam. Siku iliyofuata, Aprili 10, 2024, alishitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Anakabiliwa na shitaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, kilichotokana na maneno aliyoyatamka yanayohusiana na mpango wa kudhibiti au kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025. Mashitaka haya yamevutia umakini mkubwa wa umma na vyombo vya habari, huku wananchi wengi wakisubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama Kuu: kuachiwa huru au kuendelea kusota rumande, jambo linaloangaliwa kuwa na athari kubwa kisiasa na kisheria nchini Tanzania.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI