NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
ZANZIBAR.Mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuendelea kuwaletea wananchi wa Kaskazini Unguja maendeleo makubwa katika awamu yake ijayo ya uongozi, huku akisisitiza umuhimu wa amani, mshikamano na maridhiano kwa ustawi wa taifa.
Dkt. Mwinyi amesema kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo, kwani bila amani wananchi hawawezi kushiriki ibada, kufanya biashara wala mikutano ya kisiasa.
Amesisistiza kuwa viongozi wa CCM wataendelea kuhubiri amani kila mara na yeyote atakayevuruga utulivu wa nchi atadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa ahadi za awali, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa serikali yake imefanikiwa kujenga vituo vya afya na hospitali za wilaya katika maeneo mbalimbali, huku ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Kaskazini ukiendelea Mahonda.
Ameongeza kuwa huduma za afya zimeboreshwa kwa kuwepo kwa maduka ya dawa ndani ya hospitali hizo.
Aidha, sekta ya elimu imepiga hatua kubwa kupitia ujenzi wa shule za ghorofa za msingi na sekondari zenye vifaa vya kisasa, hali iliyoongeza ufaulu na kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Dkt. Mwinyi pia ameeleza kuwa serikali yake imewekeza kwenye miundombinu kwa kujenga barabara za lami zinazounganisha Kaskazini na Kusini, kuanza ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mangapwani, na mipango ya kuanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Nungwi.
Ameongeza kuwa miradi ya maji kupitia ushirikiano na kampuni kutoka Oman imeanza kufanikisha upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa mkoa huo.
Kwa upande wa uchumi na ajira, Dkt. Mwinyi amesema serikali itaendelea kusaidia wavuvi, wakulima na wajasiriamali kwa kujenga vituo maalumu na kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 96 kwa vikundi mbalimbali.
Ameahidi kuimarisha sekta binafsi hususan viwanda ili vijana wengi zaidi wapate ajira, pamoja na kujenga maghala ya kuhifadhi chakula, bandari ya uvuvi na viwanda vya kusarifu mwani na samaki.
Amesisitiza pia kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wa serikali kwa kuongeza mishahara na posho kadri uchumi unavyokua, huku akiahidi kujenga viwanja vya michezo katika kila mkoa na wilaya ili vijana wapate fursa ya kukuza vipaji vyao.
Dkt. Mwinyi amehitimisha lhotuba yake kwa kuwataka wananchi wa Kaskazini Unguja kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuhakikisha ushindi wa CCM, akisema.
“Tusidharau kura, kila mmoja wetu atoke akapige kura ili tuendelee kujenga Zanzibar ya mshikamano, ustawi na maendeleo.”
0 Comments