Header Ads Widget

DK KISENGE ,DK SEIF SHEKHALAGE WAONGOZA MAANDALIZI KAMBI YA MATIBABU NCHINI COMORO

 

Na Matukio Daima Media 

MADAKTARI bingwa wa hospitali tano nchini wanatarajiwa kufanya kambi ya wiki moja nchini Comoro ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilotoa wakati wa ziara yake visiwani humo.

Hospitali tano zitakazoshiriki kambi ya mwaka huu ni Benjamin Mkapa ya mkoani Dodoma, Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),  Hospitali ya Saratani ya Ocean Road,  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)  na Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI).

Madaktari watakaotoa matibabu hayo ni madaktari wa Moyo, Madaktari wa wanawake, madaktari wa saratani, madaktari wa mifupa na mishipa ya fahamu na madaktari wa figo.

Madaktari wengine ni wa mfumo wa mkojo, madaktari wa ngozi, mfumo wa maskio,pua na koo(ENT), meno na daktari wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Utalii Tiba, Dk Peter Kisenge ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakata Kikwete (JKCI).

Alisema Tanzania inategemewa zaidi na wananchi wa Comoro katika kupata huduma za sekta ya afya na kwamba idadi kubwa sana ya wananchi  wa nchi hiyo wanakuja Tanzania kwa huduma mbalimbali.

Alisema baada ya Rais Samia kuona nchi hiyo ina uhitaji mkubwa wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali  aliagiza madaktari bingwa wa Tanzania waende nchini humo kufanya kambi ya matibabu.

“Hii kambi ya Oktoba mwaka huu itafanyika katika mji wa Anjuan na mamlaka zote zinazohusika zinafanya  maandalizi ya kwenda Comoro mwezi wa kumi ,” alisema

Naye Mratibu wa Kambi hiyo, Mkurugenzi wa  Global Medicare, Abdulmalik Mollel alisema uamuzi wa Rais Samia kuagiza kufanyika kwa kambi hiyo ulitokana na  mafanikio makubwa ya kambi ya madaktari bingwa wa Tanzania iliyofanyika nchini humo mwaka 2024.

Alisema kwenye kambi hiyo iliyofanyika mji wa Moron mwaka 2024 wananchi 2,700 walihudumiwa na madaktari bingwa bobezi kutoka hospitali tano za Tanzania

 “Kwa ujumla mafanikio makubwa ya kambi iliyopita yalimfurahisha Rais  na baada ya kuombwa na wananchi wa Comoro madaktari waende tena nchini humo aliridhia  kambi kama ile ifanyike tena mwaka huu,” alisema Mollel

Alisema tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara  ya Afya wamelifanyia kazi suala la kambi hiyo na wakala wa utalii tiba Global Medicare  ndiyo inaratibu kambi hiyo kama ilivyofanya mwaka jana.

“Kambi itakuwa kuanzia tarehe 5 hadi 12 mwezi wa kumi itakuwa ya wiki moja itafanyika katika hospitali tatu za nchini humo na hospitali zetu tano zitashiriki kufanikisha kambi hiyo,” alisema

Mollel alisema Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,  Dk Seif Shekalaghe imeshatekeleza baadhi ya mambo na hospitali zitakazokwenda kule zimeshaarifiwa na zimeshateua madaktari watakaokwenda kule.

Mollel alisema tayari Wizara ya Afya imeshatuma timu ya watalaamu kutoka Tanzania kwenda nchini Comoro kwaajili ya maandalizi ya kambi hiyo ya wiki moja.

“Timu  ya wataalamu kutoka Tanzania imeshaenda kule na kukutana na wawakilishi wa Serikali ya Comoro kupitia Balozi wa Tanzania nchini humo na wamekutana na wawakilishi wa hospitali tatu zitakazotumiwa na madaktaari wa Tanzania  kutoa huduma za kibingwa,” alisema .

Aidha, Mollel alisema wamezishirikisha taasisi kubwa za kimkakati kama Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kwenye kambi ya mwaka huu MSD itatoa washiriki kwenda kwenye kambi hiyo .

“Kwenye kambi ya mwaka huu kutakuwa na maonesho na vikao vya kujengeana uwezo baina ya madaktari wetu na wale wa Comoro na kutakuwa na mkutano baina ya Bohari Kuu ya Tanzania MSD na Bohari Kuu ya Dawa Comoro kubadilishana uzoefu,” alisema.

Alisema kwenye maandalizi ya kambi hiyo ya mwaka huu wameshirikisha viwanda vya dawa hapa nchini ili viangalie fursa ya kusambaza dawa za aina mbalimbali nchini humo.

Alisema matangazo yameshafanyika kwa wananchi wa Comoro ili wafahamu  aina ya huduma ambazo madaktari wa Tanzania wanakwenda kuzitoa nchini humo.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI