Waziri wa zamani wa Cameroon na mgombea urais Issa Tchiroma Bakary anasema alizuiwa kuondoka nchini mapema leo, alipokuwa akikaribia kupanda ndege kwenda Senegal kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Yaoundé.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, alifichua kwamba alikuwa akielekea Senegal kutoa heshima zake kwenye kaburi la Rais wa kwanza wa Cameroon Ahmadou Ahidjo, ambaye alifariki katika taifa hilo la Afrika Magharibi alipokuwa uhamishoni karibu miaka 36 iliyopita.
"Nilizuiwa kiholela kupanda ndege yangu ... kufuatia maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa ofisi ya rais wa jamhuri," alisema.
Bwana Tchiroma aliongeza kuwa kitendo hicho "kinafichua uadui usiokoma wa serikali dhidi ya wagombea wanaobeba maono ya kweli na kutetea utu wa watu wetu."
Bado haijulikani ikiwa kizuizi cha kusafiri kwa Waziri wa zamani wa Kazi na Mafunzo ya Ufundi kilihusishwa tu na madhumuni ya safari yake au ikiwa kilihusishwa na marufuku ya kusafiri kwa muda usiojulikana.
Mamlaka ya Cameroon haijatoa maoni yake kuhusu tukio hilo lililomhusisha Tchiroma, ambaye pia anaongoza chama cha Cameroon National Salvation Front (CNSF).
Wakili mashuhuri wa haki za binadamu Felix Agbor Nkongho aliielezea kama "linalotia hofu sana," akisema uhuru wa watendaji wa kisiasa pamoja na wagombea urais unapaswa kuhakikishwa.
"Kukosekana kwa uwazi na utaratibu unaofaa katika suala hili kunadhoofisha imani ya umma na kuibua maswali mazito kuhusu uaminifu wa mchakato wetu wa uchaguzi," alisema.
Kizuizi hicho cha kusafiri kwa mzee huyo mwenye umri wa miaka 75 pia kinafuatia taarifa yake ya umma siku ya Jumapili, akilitaka baraza la katiba kumjumuisha kiongozi wa upinzani Maurice Kamto katika orodha ya wagombea wa kura ya urais ya Oktoba 12.
Uamuzi wa Bw. Tchiroma kutembelea kaburi la marehemu rais miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi wa urais ulizua hisia tofauti, huku wengine wakihoji wakati na nia ya kufanya matembezi hayo.
Akiwa mpinzani wa bosi wake wa zamani Paul Biya - ambaye alipinga kurejeshwa kwa mabaki ya Ahidjo kwa mazishi - wengine wanaona kitendo chake kama mkakati wa kisiasa.
0 Comments