NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
MBEYA.Waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato wametakiwa kushiriki kikamilifu Kambi la Watu Wenye Mahitaji Maalum linalotarajiwa kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza katika Mtaa wa Mlima Reli alipokuwa akihitimisha kambi la sikukuu za vibanda, Mchungaji Philibert Mwanga, Mkurugenzi wa Huduma na Shule ya Sabato wa Union, amesisitiza umuhimu wa waumini kujitoa kushiriki tukio hilo kwa ajili ya kuonesha mshikamano na upendo kwa watu wenye changamoto mbalimbali za maisha.
“Nawasihi waumini wote tuwe sehemu ya kambi hili, si kwa ibada pekee bali pia kwa kutoa msaada wa hali na mali ili kuwafariji na kuwaunga mkono ndugu zetu wenye mahitaji maalum,” alisema Mchungaji Mwanga.
Kwa upande wake, Mussa Robert Syunje, Mkuu wa Kambi lililokuwa likihitimishwa eneo hilo, amesema maandalizi ya kushiriki kambi lijalo yameanza mapema ili kuhakikisha ushiriki wa waumini kutoka maeneo mbalimbali.
“Tumeweka mikakati ya kuhamasisha washiriki kutoka makanisa yote jirani ili tufike kwa wingi na kufanya kambi la Septemba kuwa la kipekee,” alisema Syunje.
Kambi la Watu Wenye Mahitaji Maalum hufanyika kila mwaka likilenga kutoa msaada, faraja na mafundisho ya kiroho kwa walengwa, huku likiwakutanisha waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.
0 Comments