Header Ads Widget

WALIOPOTEZA KURA ZA MAONI CCM KUREJESHWA? NINI KINAFUATA?

 

Matokeo ya kura za kwa watia nia wanaowania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kugombea ubunge nchini Tanzania yameonesha kuwa zaidi ya wabunge hamsini wanaomaliza muda wao na sasa wanatetea nafasi zao wamezidiwa kura na watia nia mpya na ambao si maarufu kitaifa.

Watu maarufu zaidi kitaifa ni naibu mawaziri wasiopungua watano waliomaliza muda wao hivi karibuni, hawajaongoza kura za maoni.

Hao ni Naibu Waziri wa Malaisili na Utalii, Dunstan Ktanduala, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alex Mnyeti, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi.

Pia yumo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Geofrey Pinda na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe.

Kwa upande wa wabunge waliomaliza muda wao hivi karibu na waliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini, miongoni mwao ni pamoja na Charles Mwijage aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili, Hamis Kigwangala na aliyewahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Isack Kamwelwe na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa elimu,Stella Manyanya.

Pia yumo Deo Sanga ambaye amekuwa mbunge wa Makambako kwa zaidi ya vipindi vitatu.

Haya ni matokeo ya kura za maoni ambayo hayakutarajiwa na wengi.

Sasa watia nia wote walioongoza na wengineo watakuwa wanangojea maoni ya vikao vya chama kuanzia ngazi ya kamati za siasa za wilaya kwa Tanzania Bara, na kamati maalumu kwa Zanzibar Mkoa, Kamati Kuu ya CCM Taifa hadi Halmashauri Kuu ya Taifa iliyopangwa kuketi Agosti 20, kupendekeza majina ya mwisho yatakayopelekwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Ifahamike kuwa si wote wanaooongoza huteuliwa kuwa wagombea. Wakati fulani aliwahi kuteuliwa hadi mtu aliyeshika nafasi ya nne.

Wabunge wengine walioangushwa kura za maoni

Katika Jimbo la Vunjo, Dr. Charles Kimei ameanguka, Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amepoteza mbele ya Moris Makoi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi. Katika Jimbo la Iringa Mjini, aliyekuwa mbunge Jesca Msambatavangu amejikuta nafasi ya nne kwa kura 408. Mshindi wa kura hizo ni Fadhil Ngajilo aliyepata kura 1,899.

Kyerwa, Mbunge Innocent Bilakwate ameangushwa na Khalid Nsekela aliyezoa kura 5,693 sawa na asilimia 71 huku Bilakwate akipata kura 1,567.

Tabora Mjini, Shabani Mrutu ameongoza kwa kura 6,612, akimshinda kwa mbali aliyekuwa mbunge Emmanuel Mwakasaka aliyepata kura 228 pekee.Katika jimbo la Namtumbo, aliyekuwa Mbunge Vita Kawawa ameshindwa mbele ya Dkt. Juma Zuberi Homera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Mtwara Mjini, Joel Arthur Nanauka ameibuka mshindi kwa kura 2,045 dhidi ya Hassan Mtenga Mbunge anayemaliza muda wake aliyepata kura 1,607.

Katika Jimbo la Lindi Mjini, Mbunge anayemaliza muda wake, Hamida Abdalla, ameangushwa na Mohamed Utali

Nini kinafuata baada ya kura za maoni?

Wajumbe wamepiga kura ya maoni kueleza kwa vitendo wanamtaka nani, lakini CCM inazitaja sifa hizi za uongozi kama muhimu kwenye kumtafuta mwakilishi wa chama hicho.

Hata hivyo, uamuzi wa wajumbe umetuma ujumbe mzito kwamba mabadiliko yanahitajika, na sura mpya zinaungwa mkono. Kwa waliokuwa wabunge waliokataliwa na wanachama wao, matumaini pekee yaliyobaki ni uamuzi wa huruma kutoka juu kama utakuwepo.

Je, vikao vya juu vitarejesha majina yaliyokataliwa na msingi wa chama, au vitaacha sauti ya wajumbe iwe sauti ya wananchi? Macho na masikio sasa yako Dodoma.

Sasa hatua muhimu itakayofuata ni Kamati za Siasa za Kata/Wadi kuwajadili wagombea udiwani na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Jimbo/Wilaya. Huku Vikao vya Kamati za Utekelezaji za UWT Wilaya vitawajadili wagombea Udiwani wa Viti Maalum na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

Nayo Kamati ya Siasa ya Jimbo inafanya vikao kuwajadili wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Wadi kwa upande wa Zanzibar na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

Baada ya hapo mapendekezo yataenda ngazi ya mkoa, ambapo Kamati za siasa za mikoa zitajadili wagombea Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoa mapendekezo kwa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.

Kikao cha Halmashuri Kuu ya CCM ya Taifa ndiyo ngazi ya mwisho ambayo itafikiria na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo na Viti Maalum.

Kwa waliokuwa wabunge waliokataliwa na wanachama wao kupitia kura za maoni, matumaini pekee yaliyobaki ni uamuzi wa huruma kutoka vikao hivi vya juu kama utakuwepo.

Je, vikao vya juu vitarejesha majina yaliyokataliwa na msingi wa chama, au vitaacha sauti ya wajumbe iwe sauti ya wananchi? Macho na masikio sasa yako Dodoma.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI