Header Ads Widget

TIRA YAHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA BIMA KULINDA SHUGHULI ZA KILIMO, MIFUGO, UVUVI NA MISTU.

Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Richard Toyota akizungumza juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya mifungo, uvuvi, Misitu na kilimo

Na Chausiku Said,Matukio Daima,

 MWANZA.Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesema kuwa serikali imejiwekea lengo ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa wa bima na angalau asilimia 50 wawe wanatumia huduma hizo, ikiwa ni mkakati wa kulinda rasilimali na kukuza uchumi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 5, 2025 katika maonesho ya Nane Nane yanayofanyikakwenye viwanja vya Nyamohongolo jijini Mwanza, Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Richard Toyota, alisema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa taasisi hiyo kutoa elimu ya bima kwa wananchi hususani wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wadogo.

Toyota akisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya kufuatia sheria iliyosainiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2023 kuhusu bima ya afya kwa wote.

Afisa Bima  kutoka NIC Insurance Alphonce Paul akielezea namna ambavyo bima ya mifugo, inavyoweza kumnufaisha mfugaji pindi anapokuwa amekata bima hiyo.

“Tunawahamasisha wananchi, taasisi na watoa huduma kusajiliwa na TIRA ili mifumo ya bima ifanye kazi kwa ufanisi. Pia tupo hapa kusaidia wajasiriamali na wananchi wanaotaka kuwa mawakala au madalali wa bima kusajiliwa moja kwa moja,” alisema Toyota.

Aliongeza kuwa licha ya Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70 kutegemea kilimo, mifugo, uvuvi na misitu, bado huduma za bima kwenye sekta hiyo haijapenya ipasavyo, Alisema kwa Kanda ya Ziwa pekee, takribani watu milioni 9.8 wanajihusisha na shughuli hizo, lakini idadi ya walioweka bima ni chini ya milioni 5.

Afisa Bima kutoka Reliance Insurance jijini Mwanza, Endrew Gabana akielezea umuhimu wa kuwa na bima ya kilimo inayolenga kumlinda mkulima dhidi ya majanga ya ukame, magonjwa, wadudu na mvua nyingi

“Serikali imechukua hatua madhubuti, mfano mpango wa utambuzi wa mifugo uliozinduliwa Juni 16, 2025 na Rais Samia kupitia mfumo huo, mifugo inaweza kutambuliwa kidijitali, hivyo kurahisisha utoaji wa bima,” alisema Toyota.

Aidha, alieleza kuwa bima za kilimo na mifugo sasa zinaweza kutolewa kwa uhakika zaidi kutokana na uwepo wa skimu mbalimbali za serikali kama BBT na TWAISI, zinazosaidia kupunguza hatari zinazowakatisha tamaa wakulima na wafugaji.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI