Header Ads Widget

VIJANA WATAKIWA KUIBEBE AJENDA YA UTALII DODOMA, KIJIJI CHA UTALII KUZINDULIWA KAMA KIVUTIO KIPYA

 

VIJANA wametajwa kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya sekta ya utalii nchini, hasa katika Mkoa wa Dodoma, ambao sasa unaelekezwa kuwa kitovu cha utalii wa ndani kwa kuzingatia fursa na vivutio lukuki vilivyopo. 


Wito huo umetolewa wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kukuza utalii mkoani humo, ambapo vijana wamehimizwa kuonesha ubunifu, kutumia teknolojia na kuanzisha miradi ya kitalii ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo kwa manufaa ya taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Selemani Jafo amesema kuwa vijana wa Dodoma wana nafasi ya kipekee ya kuongoza mapinduzi ya utalii kutokana na uwezo wao wa kuhimili mabadiliko na kutumia majukwaa ya kidijitali kutangaza vivutio vya nchi.

Ameeleza kuwa kupitia ajenda hiyo, vijana wanaweza kuanzisha makampuni ya kuongoza watalii, kutoa huduma za malazi na chakula, na kushiriki katika maonesho ya sanaa na utamaduni.

Amesema katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kwa kasi na kwa tija, mkakati huo umeweka msisitizo wa kuanzishwa kwa kijiji maalum cha utalii katika Mkoa wa Dodoma.

"Kijiji hicho kitakusanya vivutio vya kitamaduni, kisanaa na vya asili na kuwa jukwaa la kudumu la kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi," Amesema Waziri Jafo kwaniab ya Waziri mkuu . 

Aidha Waziri Jafo amesema , kijiji hicho kinatarajiwa kutoa fursa za ajira, biashara na mafunzo kwa vijana, huku kikihifadhi urithi wa kihistoria na kitamaduni wa mkoa huo.

Pia Viongozi huyo ametaja vivutio vya kipekee vya Dodoma kama vile Hifadhi ya Mkungunero, maeneo ya kihistoria, na uzalishaji wa zabibu bora zinazotumika kutengeneza juisi na mvinyo. 

"Inasemekana kuwa zabibu tamu za Dodoma na mchuzi wake wa asili ni hazina inayoweza kuibuliwa zaidi kwa kuhamasisha utalii wa kilimo na chakula," Amesema .

Akielezea Reli ya kisasa ya SGR amesema kuwa miongoni mwa vivutio vipya vinavyochangia kuimarika kwa sekta ya utalii, stesheni ya Dodoma ambayo  inatajwa kuvutia wageni wengi wanaoshuka kwa ajili ya kupiga picha, kushiriki maonesho au kupata huduma mbalimbali zinazotolewa mkoani humo.
Amesisitiza kuwa mpango huu haupaswi kubaki kwenye makaratasi bali utekelezwe kwa kasi ili kuhakikisha Dodoma inanufaika ipasavyo na rasilimali zake za kitalii.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa sekta binafsi, wawekezaji na taasisi za elimu kushirikiana na serikali katika kutekeleza mkakati huu kwa vitendo. 

Amesema mkakati huo pia unaweka kipaumbele katika kuunganisha sekta ya kilimo na utalii, maarufu kama ambapo mazao kama zabibu, vyakula vya asili, na usindikaji wa bidhaa vilikuwa sehemu ya vivutio kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

"Kupitia mpango huu, Dodoma inatarajiwa kuibuka kama moja ya maeneo ya mfano katika utalii wa ndani na wa kimataifa, huku vijana wakipewa nafasi ya kuwa mabalozi wa utalii na wahusika wakuu katika kulinda na kutangaza utajiri wa taifa," Amesema.

Uzinduzi wa mkakati huo umefanyika kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi, ukiwa na lengo la kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa Dodoma kupitia fursa za kiuchumi, ajira na uwekezaji.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI