Serikali wilayani Same imesema itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na mashirika binafsi katika kuendelea kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha jamii kutunza na kuhifadhi mazingira, ikiwemo kufanya shughuli za upandaji miti hasa miti ya asili pamoja na ufugaji wa nyuki.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, alipokuwa akitembelea kitalu cha miche ya miti kilicho chini ya mradi wa uhifadhi na urejeshaji asilia kwa kupanda miti ya asili kwa njia shirikishi, uliopo kijiji cha Vumari na unatekelezwa na asasi isiyo ya kiserikali iitwayo Climate Action Network (CAN).
Mhe. Kasilda amesema ujio wa mradi huu ni ukombozi wa mazingira kwani maeneo mengi wananchi wamekata miti ya asili iliyokuwepo awali, hivyo jitihada hizi zitasaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Maeneo mengi miti ya asili imekatwa kwa ajili ya matumizi ya nishati ikiwemo kuni, hivyo ujio wa mradi huu ni dhahiri kuwa tunakwenda kurejesha miti ya asili iliyokuwa imekatwa kwa sababu wananchi walikosa elimu kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira,” alisema Mhe. Kasilda.
Pia amewasisitiza wananchi kushirikiana na shirika hilo ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu kwa manufaa mapana ya wilaya ya Same pamoja na Taifa kwa ujumla kwani kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi kutoka Climate Action Network (CAN), Bi. Sharon Kishenyi amesema mpaka sasa wamefanikiwa kutoa elimu ya uhifadhi kwa kiwango kikubwa katika maeneo yaliyoathirika na ukataji wa miti ya asili huku zaidi ya miti 60,000 ikiwa tayari imepandwa kwenye maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa.
Hata hivyo, amesema mradi huo ulianzishwa mahsusi kwa lengo la kuhimiza, kuelimisha na kuwezesha jamii katika uhifadhi na urejeshaji wa miti ya asili pamoja na ufugaji wa nyuki, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo ulianza kutekelezwa juni 2021 katika wilaya ya mbili ya Same Mkoani Kilimanjaro na Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga kwa sasa utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho kumalizika ifikapo Septemba mwaka huu.
0 Comments