Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
MSIBA wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Ndugai, umegeuka kuwa jukwaa la kusherehekea mafanikio na kumbukumbu ya maendeleo aliyoyaacha, hasa katika jimbo lake la Kongwa.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwaongoza waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana, alihamisha mtazamo kutoka kwenye majonzi kwenda kwenye urithi wa maendeleo ambao Hayati Ndugai aliufanikisha akiwa kiongozi.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema kuwa mbali na kuwa kiongozi wa mhimili wa Bunge, Ndugai alitumia nafasi yake kupigania maendeleo ya wananchi wake wa Kongwa kwa juhudi na bidii kubwa, akitumia nafasi yake kama mbunge na Spika kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu wa kawaida.
“Kongwa ya leo siyo ya mwaka 2000. Leo kuna shule nyingi zaidi, zahanati nyingi zaidi, vituo vya afya, na vijiji vyote vina umeme. Hili ni jambo kubwa sana,” alisema Dk. Samia huku akibainisha kuwa maendeleo hayo hayakuja kwa bahati, bali kwa msukumo wa dhati wa marehemu.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Rais, shule za msingi katika Kongwa zimeongezeka kutoka 50 mwaka 2000 hadi 131, na shule za sekondari kutoka 3 hadi 45. Zahanati zimefikia 56 kutoka 12, na vituo vya afya sasa vipo 10 kutoka vitatu.
Viongozi mbalimbali walitumia jukwaa hilo kuonesha namna Ndugai alivyoacha alama si tu kitaifa bali katika mkoa wa Dodoma, huku wengine wakihusisha mafanikio yake na msukumo wa maendeleo ya elimu na sekta ya afya.
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, aligusia historia ya Ndugai kama mtu aliyekulia kwenye mazingira ya unyonge lakini hakuyafanya kuwa kikwazo cha kupanda hadi nafasi ya juu ya uongozi. Alisema alikuwa na msukumo wa kuwasaidia vijana kupata elimu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Miongoni mwa waliohudhuria msiba huu, wapo vijana waliopata elimu ya juu kwa sababu ya jitihada binafsi za Hayati Ndugai,” alisema Rais Samia, akiongeza kuwa marehemu alisimamia ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge, iliyopo Kikombo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na Jaji Mkuu, George Masaju, walimuelezea marehemu kama mpenda haki, aliyeamini katika utawala bora, na aliyesimamia vizuri matumizi ya rasilimali za taifa kupitia kamati maalum za ushauri bungeni.
Katika uhai wake, Ndugai aliwahi kuanzisha kamati nne za bunge zilizoangazia udhibiti wa rasilimali kama almasi, Tanzanite, gesi asilia na uvuvi wa bahari kuu. Mapendekezo ya kamati hizo yalisadia kuongeza mapato ya serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema kuwa mchango wa Hayati Ndugai katika mapinduzi ya elimu na kilimo katika mkoa huo hautasahaulika. Alisema alihimiza kilimo cha korosho na kuhimiza vijana kujiajiri kupitia sekta hiyo.
Kwa ujumla, tukio hilo limekuwa zaidi ya kutoa heshima kwa marehemu limekuwa ni kumbukizi ya mchango wa mtu mmoja aliyekuwa na maono, aliyewasha moto wa maendeleo kijijini na kitaifa, na ambaye historia haitamsahau kwa alama alizoziacha.
"Mchango wa Kongwa katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika ni urithi mkubwa hayati Ndugai alitamani kuanzishwa kwa makumbusho ya taifa na eneo hilo kuwa sehemu ya utalii wa kihistoria," alisema Dk. Samia, akihitimisha kwa kuhimiza kuendelezwa kwa maono ya marehemu.
Mwili wa Hayati Ndugai unasafirishwa leo kuelekea kijijini kwao Seleje, wilayani Kongwa, kwa maziko.
0 Comments