Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
KAMPUNI ya RIJKZWAAN Tanzania imepata mafanikio makubwa kupitia uzalishaji wa mbegu bora, zenye tija na rafiki kwa mazingira jambo ambalo limewawezesha wakulima wengi nchini kuongeza uzalishaji kwa uendelevu huku wakilinda mazingira yao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima na wafugaji kwenye viwanja vya Nzuguni Nanenane Dodoma Naiman Mollel, Afisa Kilimo wa RIJKZWAAN Tanzania, alisema kuwa mbegu hizo zimebuniwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mimea, na uhitaji wa uzalishaji mkubwa kwa kutumia njia salama na endelevu.
“Mbegu tunazozalisha si tu kwamba ni bora kwa mavuno, bali pia ni salama kwa mazingira Zimeundwa mahsusi kuhimili hali ngumu ya hewa na kusaidia wakulima kupata mazao bora bila kuathiri mazingira yao,” alisema Mollel.
Aidha, aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kuwakaribisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini kushirikiana nao katika safari ya kilimo chenye tija na kinacholinda mazingira.
“RIJKZWAAN imejipanga kuwa mshirika wa kweli kwa wakulima wa Tanzania kwa kuwapatia mbegu bora, elimu ya kilimo bora, na kuwawezesha kupata mavuno ya uhakika kwa njia rafiki kwa mazingira,” alisisitiza.
Mbegu za RIJKZWAAN zimepokelewa kwa mikono miwili na wakulima kutoka mikoa mbalimbali kutokana na uwezo wake wa kustahimili magonjwa, kutoa mazao mengi, na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mwisho
0 Comments