Na Matukio Daima Media
Mgombea ubunge wa Jimbo la Isman kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), William Vangimembe Lukuvi,na mbunge ubunge jimbo la Kalenga Jackson Gidion Kiswaga leo tarehe 27 Agosti 2025 wamerejesha rasmi fomu ya kuwania nafasi ya ubunge kwa muhula mwingine, baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Zoezi hilo lilifanyika kwa utaratibu mzuri na wa kistaarabu, huku likiwa ni ishara ya mwanzo wa safari nyingine ya kisiasa kwa Lukuvi katika kuliongoza tena Jimbo la Isman na Kiswaga kuongoza jimbo la Kalenga.
Lukuvi, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wenye uzoefu mkubwa nchini, aliwasili katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi akiwa ameambatana na mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Gidion Kiswaga.
Wote wawili waliambatana na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya ya Iringa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa, Costandino Kihwele Kama ilivyoelekezwa na Tume ya Uchaguzi, msafara huo ulitumia magari sita tu, na haukuwa na shamrashamra kama ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma, jambo ambalo linaashiria ukomavu wa kisiasa na heshima kwa kanuni na taratibu za uchaguzi.
Kwa Lukuvi, kurejesha fomu hiyo si jambo jipya, lakini ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu ya kuendelea kutumikia wananchi wa Jimbo la Isman anaingia katika kinyang’anyiro hiki akiwa na matumaini makubwa ya kupata ridhaa ya wananchi tena, kutokana na kazi kubwa alizozifanya katika awamu zilizopita alipokuwa mbunge wa eneo hilo.
Rekodi ya Mafanikio Jimboni Isman
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Lukuvi ameweka historia ya kipekee katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Jimbo la Isman limeona mabadiliko makubwa, hasa katika sekta ya elimu, miundombinu ya barabara, miradi ya umwagiliaji, na huduma ya maji safi.
Ikumbukwe mojawapo ya mafanikio makubwa ambayo wananchi wa Isman wanayakumbuka ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika Bonde la Pawaga, ambayo imeongeza tija kwa wakulima na kuinua pato la kaya nyingi.
Pia, katika sekta ya elimu, shule nyingi zimejengwa na nyingine kukarabatiwa, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia.
Idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari kwa mafanikio imeongezeka, jambo linaloashiria kuwa juhudi zake zimezaa matunda.
Pia sekta ya afya haikubaki nyuma, kwani vituo vya afya vimeboreshwa, na huduma zimekaribia zaidi wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospital ya wilaya eneo la Pawaga.
Chuo cha ufundi stadi (VETA) Kilichojengwa Pawaga kimekuwa chachu kubwa kwa wananchi hasa vijana kupata ujuzi.
Changamoto ya muda mrefu ya maji safi katika Tarafa ya Ismani sasa imepatiwa ufumbuzi wa kudumu. Miradi ya maji iliyotekelezwa imerahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa maeneo mengi, jambo linalowapa matumaini makubwa wananchi kuwa kama wataendelea kumpa ridhaa Lukuvi, changamoto nyingine zilizobaki zitapatiwa suluhisho.
Uungwaji Mkono Kutoka Kwa Viongozi
Kurejeshwa kwa fomu ya Lukuvi kumeonyesha pia mshikamano mkubwa wa kisiasa ndani ya CCM, hasa katika Mkoa wa Iringa.
Uongozi wa chama katika wilaya hasa kamati ya siasa ya wilaya walijitokeza kuwaunga mkono, jambo linaloashiria kuwa Lukuvi si mgombea binafsi, bali ni sehemu ya timu yenye malengo ya pamoja ya kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa, Costandino Kihwele, alisisitiza kuwa chama kinamuunga mkono kikamilifu Lukuvi na Kiswaga ndio wagombea wao kutokana na ufanisi wao katika kutekeleza majukumu ya uwakilishi.
Lukuvi aliwashukuru wananchi wa Isman ambao walitamani kumsindikiza kwa wingi Ila taratibu za tume haziruhusu shamla shamla hivyo kuwaomba mapenzi Yao kwake wahamishie kwenye box la kura na kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni wakati akiomba kura za madiwani na za Rais Dkt Samia .
Alieleza kuwa kazi aliyofanya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati yake na wananchi, pamoja na viongozi wa serikali katika ngazi zote ndio maana kila hatua wananchi wa Isman wanatamani kumuunga mkono hivyo juu ya nini atawafanyie atasema muda wa kampeni sio leo.
Mgombea wa Kalenga
Sambamba na Lukuvi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Gidion Kiswaga, naye alirejesha fomu yake ya kugombea ubunge kwa muhula mwingine.
Kama ilivyo kwa Lukuvi, Kiswaga amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Kalenga.
Katika kipindi chake cha uongozi, Kiswaga ameweza kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara na upatikanaji wa maji safi.
Jimbo la Kalenga, ambalo zamani lilikuwa likikabiliwa na matatizo ya miundo mbinu duni na huduma hafifu za kijamii, sasa limebadilika kwa kiasi kikubwa.
Kiswaga amehakikisha kuwa barabara nyingi zinapitika wakati wote wa mwaka, huku miradi ya maji ikiwafikia wananchi katika maeneo ambayo kwa miaka mingi walikuwa wakitegemea vyanzo visivyo salama.
Aidha, Kiswaga amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia miradi ya afya na elimu, akihakikisha kuwa watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu, huku akinusuru maisha ya wananchi kupitia uboreshaji wa huduma za afya.
Ushirikiano na Serikali Kuu
Lukuvi na Kiswaga wote wawili wamekuwa wakisisitiza kuwa mafanikio ya majimbo yao yamewezeshwa na ushirikiano mzuri na Serikali Kuu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo umechochewa na dhamira ya Rais Samia ya kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi, pamoja na ufuatiliaji mzuri wa viongozi wa majimbo kwa kushirikiana na watendaji wa serikali.
Dkt. Samia, ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa uchaguzi ujao, ameendelea kupigiwa chapuo na viongozi hao wawili kutokana na mafanikio makubwa ya serikali yake katika kipindi cha uongozi wake.
Lukuvi na Kiswaga wamesisitiza kuwa ushindi wao hautakuwa wa mtu binafsi, bali ni ushindi wa CCM na dhamira yake ya kuendelea kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.
Kurejeshwa kwa fomu na wagombea hawa wawili ni sehemu ya hatua muhimu za kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Wananchi wa Isman na Kalenga sasa wana nafasi ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kufanya maamuzi ya busara yatakayowapa mwendelezo wa maendeleo.
Kwa historia ya utendaji wao, Lukuvi na Kiswaga wanaingia kwenye kinyang’anyiro hiki wakiwa na matumaini makubwa ya kurejea bungeni, wakibeba ndoto, matumaini na matarajio ya maelfu ya wananchi waliowachagua hapo awali.
0 Comments