MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amesema kuwa ukuaji wa sekta ya fedha nchini ikiwemo mabenki yamekuwa kichocheo kikubwa cha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Dk.Mpango alisema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa benki ya CRDB tawi la Buhigwe na kusema kuwa benki hiyo imekuwa moja ya mabenki yaliyoweza kutoa fedha za kuanzishwa kwa miradi mikubwa nchini na hivyo kuifanya miradi kuanza na kwendaa kwa kasi.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa uzalishaji umeme katika bwawa la Mwalim Nyerere (MNHP) ambapo kabla haijapatikana pesa ya kuanzisha miradi hiyo benki hiyo ilitoa fedha na miradi ikaweza kuanza na kwamba benki hiyo imesaidia katika kutekelezaa miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Sambamba na hilo Makamu huyo wa Raisi alisema kuwa benki hiyo imekuwa kichocheo kikubwa katika kukuza diplomasia ya uchumi kwa kuwezesha kufungua matawi katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) ambapo Watanzania wamekuwa wakifanya biashara, uwekezaji na shughuli za kiuchumi na nchi hizo ambapo pia imeimarisha mahusiano baina ya nchi hizo.
Aidha Dk.Mpango alisema kuwa kufunguliwa kwa matawi ya benki katika mikoa mbalimbali nchini na wilayani imekuwa kichocheo katika kukuza biashara na shughuli za kiuchumi za wananchi wa kawaida ikiwemo vijijini ambapo wananchi pamoja na kufanya miala lakini wameweza kukopa, kuanzisha na kuendelesha shughuli zao za biashara na uchumi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa huduma za kibenki za benki hiyo zimekuwa na kuifanya kuwa benki ya tatu kwa ukubwa katika nchi za Afrika Mashariki ambapo imeweza kuunga mkono sera na mipango ya serikali katika maendeleo na kukuza uchumi ikiwa na matawi 260 nchini .
Alisema kuwa mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya fedha yameiwezesha benki hiyo kujitanua na kutekeleza diplomasia ya uchumi ambapo kwa sasa benki hiyo ina matawi katika nchi za Burundi na DRC na iko mbioni kufungua tawi katika nchi za Falme za kiarabu.
Nsekela alisemaa kuwa kutokana na kazi nzuri na mazingira mazuri yaliyowekwa imeweza kuongeza faida kutoka kiasi cha shilingi Bilioni 371 na kufikia Bilioni Zaidi ya 500 mwaka jana ambapo kwa nusu mwaka wa mwaka huu imeweza kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 351 kama faida.
0 Comments