Moses Ng’wat, Mbozi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amesema kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali mkoani humo inaridhisha, jambo alilolihusisha moja kwa moja na juhudi za wananchi kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano kubwa la wajasiriamali lililofanyika Agosti 26, 2025 katika viwanja vya stendi ya malori mjini Vwawa, Wilaya ya Mbozi, RC Makame alisema serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wadogo ili kukuza uchumi jumuishi.
“Serikali inatambua kuwa watu wengi wamejiajiri kupitia shughuli kama bodaboda, bajaji, mama lishe, baba lishe, na machinga, ndio maana tumeamua kusogeza huduma na fursa karibu nao kwa njia rahisi ili waweze kujitegemea zaidi,” alisema Makame.
Kongamano hilo lilikutanisha mamia ya wajasiriamali na wadau wa maendeleo ya uchumi wa kati na chini, kwa lengo la kutoa mafunzo ya kuongeza maarifa ya kifedha, kukuza mitaji, na kuhamasisha matumizi sahihi ya mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri na benki ya NMB.
“Songwe ni mkoa mpya lakini maendeleo yanayoonekana ni makubwa hasa katika kilimo na biashara, kutokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wananchi,” aliongeza.
Aidha, Rc Makame alikumbusha kuwa Rais Samia ameelekeza asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kuendeleza mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, huku serikali ikiweka fedha maalum NMB kwa ajili ya mikopo nafuu.
Katika hotuba hiyo, RC Makame alitumia nafasi hiyo pia kugusia mafanikio katika sekta ya elimu wilayani Mbozi, lakini akaonyesha masikitiko yake kuhusu mimba za utotoni ambazo bado ni changamoto kubwa.
“Watoto wa kike wakipewa nafasi ya kusoma hadi kufikia ndoto zao, watachangia sana maendeleo ya familia na taifa hivyo tunapaswa kukomesha kabisa mimba za utotoni,” alisisitiza.
Alimaliza kwa kuwasihi wajasiriamali waliopata mafunzo hayo kutumia maarifa hayo katika kukuza biashara zao, kutunza mitaji, na kuhakikisha wanakuwa mfano bora kwa jamii.
0 Comments