Header Ads Widget

ZAIDI YA WATAALAMU 700 WA RASILIMALIWATU KUKUTANA ARUSHA

  

Na Pamela Mollel,Arusha 

Zaidi ya wataalamu 700 wa usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala kutoka taasisi mbalimbali za umma nchini kukutana jijini Arusha kwa ajili ya kujadili mwelekeo mpya wa utendaji kazi unaolenga kuendana na kasi ya mageuzi ya teknolojia na mabadiliko ya mahitaji ya huduma kwa umma.


Mkutano huo mkubwa wa kitaifa unatarajiwa kuwapa nafasi wataalamu hao kuchambua kwa kina namna bora ya kuimarisha ufanisi katika taasisi za umma kupitia mifumo ya kisasa ya utawala na matumizi ya TEHAMA. Wataalamu hao watashiriki katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPA-HR), utakaofanyika kuanzia Julai 22 hadi 25, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, chini ya kaulimbiu: "Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala: Kusukuma mabadiliko, kuendana na mageuzi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha huduma katika utumishi wa umma."


Akizungumza na waandishi wa habari Julai 18, 2025 jijini Arusha, Mwenyekiti wa TAPA-HR, Grace Meshy, alisema mkutano huo ambao ni wa kwanza kufanyika nchini, utafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene.


Meshy alisema kuwa mkutano huo ni sehemu muhimu ya mkakati wa kujiandaa kukabiliana na mazingira ya utendaji yanayobadilika kwa kasi, hasa katika nyanja za kidijitali, ili kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.


“Kasi ya mabadiliko ya teknolojia inaonyesha wazi kuwa kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu wenye uwezo wa kuendana na mabadiliko hayo ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Meshy.


Aidha, alieleza kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa la kipekee kwa wataalamu hao kujifunza, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma kwa lengo la kuleta mageuzi chanya katika taasisi za umma.


Kwa mujibu wa Meshy, mkutano huo pia unatarajiwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha weledi, maadili, na mifumo ya kiutendaji miongoni mwa wataalamu wa kada ya rasilimaliwatu na utawala nchini.


Naye Katibu wa TAPA-HR, Prisca Lwangili, alisema mkutano huo utahusisha mada mbalimbali zenye lengo la kuboresha mbinu bora za kiutawala, kuimarisha uongozi, matumizi ya TEHAMA, na kukuza uwajibikaji katika sekta ya umma.


“Tunaomba waajiri kutoka wizara, mamlaka za serikali za mitaa, wakala wa serikali, mashirika ya umma, vyuo vikuu na taasisi nyingine za umma kuhakikisha wanawawezesha wataalamu wao kushiriki katika mkutano huu, kwani ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa maendeleo ya rasilimaliwatu na utawala bora,” alisema Prisca.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI